1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron, Scholz waepuka kutaja mauaji ya Ukraine kuwa halaiki

Sylvia Mwehozi
14 Aprili 2022

Viongozi wa Ufaransa na Ujerumani wamekataa kurejelea kauli aliyoitoa rais wa Marekani Joe Biden kwamba Urusi inatekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Ukraine na kuonya kwamba kauli kama hizo haziwezi kukomesha vita.

https://p.dw.com/p/49ut8
Bilderchronik des Krieges in der Ukraine
Picha: Rodrigo Abd/AP/picture alliance

Biden alivituhumu vikosi vya rais Vladimir Putin kwa kufanya mauaji ya halaiki, akisema "ilikuwa ni wazi kwamba Putin anajaribu kuondoa wazo la hata kuwa raia wa Ukraine".

Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau naye amekubaliana na hoja ya Biden akisema ni "sahihi" kuelezea mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine kama mauaji ya kimbari. Lakini wakati akizungumza na kituo cha France 2, rais Emmanuel Macron amesema viongozi wanapaswa kuwa makini na lugha wanayotumia. Macron alikwenda mbali na kusema kwamba ni bora kuwa na "uangalifu wa kutumia neno la mauaji ya kimbari katika hali ya sasa" haswa kutokana na undugu na ukaribu wa Urusi na Ukraine.Urusi yalaumiwa kwa ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu nchini Ukraine.

Hata hivyo rais wa Ukraine Volodmyr Zelensky alilaani mara moja hatua ya Macron kushindwa kuyatambua mauaji ya nchini mwake kama ya kimbari. Naye Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz pia alizungumzia uhalifu wa kivita nchini Ukraine lakini alijiepusha na kutaja mauaji ya halaiki. Alisema "hii ni vita mbaya mashariki mwa Ulaya. Uhalifu wa kivita unatendeka". Kansela Scholz pia alitolea ufafanuzi wa kwamba hana dhamira ya kuzuru Ukraine katika siku za hivi karibuni, ingawa amekuwa katika mawasiliano ya mara kwa mara na rais Zelensky.

Ukraine | Fünfer-Gipfel in Kiew
Rais zelenksy na viongozi wa Poland, Lithuania, Latvia na EstoniaPicha: Ukrainian Presidential Press Office/AP/picture alliance

Hayo yakijiri marais wa Poland, Lithuania, Latvia na Estonia siku ya Jumatano walikutana na rais Zelensky mjini Kyiv na kutoa wito wa msaada zaidi wa silaha kwa ajili ya Ukraine na kutaka pia Urusi kuwajibishwa kutokana na matendo yake. Kabla wakutane na Zelensky, marais hao wanne walitembelea maeneo ya mjini Kyiv ambako mamia ya raia wanadaiwa kuuwawa baada ya miili kugunduliwa.

Nayo wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema siku ya Jumatano kwamba zaidi ya wanajeshi 1,000 wa Ukraine wa kikosi cha wanamaji wamejisalimisha katika mji wa bandari wa Mariupol.Taarifa hizo zinaashiria kwamba sasa vikosi vya Urusi huenda vimekaribia kuudhibiti mji huo ambao umekuwa ukilengwa katika eneo la mashariki mwa Ukraine. Kukamatwa kwa wilaya ya Azovstal ambayo ni ya kiviwanda kutaipatia Urusi udhibiti kamili wa Mariupol, mji ambao ndio wenye bandari kubwa katika bahari ya Azov, na pia kuanzisha njia ya kusini kabla ya mashambulizi mengine yanayotarajiwa upande wa mashariki.

Kwingineko raia wanne wameuawa na wengine 10 kujeruhiwa katika mji wa pili kwa ukubwa wa Kharkiv katika eneo la mashariki mwa Ukraine. Meya wa mji huo alithibitisha taarifa za raia kuuwawa kupitia televisheni ya taifa.

Ukraine | Zerörtes Theater in Mariupol
Hali katika mji wa bandari wa MariupolPicha: Alexander Nemenov/AFP/Getty Images

Katika hatua nyingine rais Joe Biden ameidhinisha kiasi cha dola milioni 800 kama msaada mpya wa kijeshi kwa Ukraine. Msaada huo unajumuisha mifumo ya mizinga ya ardhini na helikopita kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wake dhidi ya mashambulizi makali ya Urusi upande wa mashariki. Biden ametangaza msaada huo baada ya kufanya mazungumzo kwa njia ya simu na rais Zelensky na kuelezea kwamba Marekani itaendelea kufanya kazi na washirika wake ili kuisadia Ukraine na silaha zaidi pamoja na rasilimali nyingine wakati mzozo ukiendelea.Putin asema malengo yake Ukraine yatafanikiwa

Na katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema haoni uwezekano wa "usitishaji mapigano nchini Ukraine" akiashiria kwamba Umoja wa Mataifa bado unasubiri majibu kutoka Urusi juu ya mapendekezo ya kuwahamisha raia na usambazaji wa misaada. Hivi karibuni, Guterres alimtuma mkuu wa ofisi ya misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths mjini Moscow na Kyiv kwa lengo la kuhimiza usitishaji mapigano.