1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN, Marekani zawataka Wahouthi kusitisha mashambulizi Marib

17 Februari 2021

Umoja wa Mataifa na Marekani wamewatolea wito waasi wa Kihouthi kusitisha mashambulizi dhidi ya mji wa kati mwa Yemen wa Marib wenye utaji wa mafuta, wakisema mashambulizi hayo yanaweza kuhatarisha mamilioni ya raia.

https://p.dw.com/p/3pTYu
Jemen Militär starte Offensive gegen Houthi-Rebellen ARCHIV
Picha: picture alliance/dpa/Str

Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran walianzisha tena mashambulizi yenye lengo la kuuteka mji wenye utajiri wa mafatu wa Marib ulioko umbali wa kilomita 120 mashariki mwa mji mkuu, Sanaa unaoshikiliwa na waasi hao.

Soma pia:Wahouthi washambulia viwanja vya ndege vya Saudi Arabia

Kuanguka kwa mji huo litakuwa pigo kubwa kwa serikali ya Yemen, inayoungwa mkono na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, lakini pia kunatishia kusababisha janga kwa raia, wakiwemo mamia kwa maelfu ya watu walioachwa bila makazi wanaohifadhiwa katika makambi yaliyotelekezwa mjini humo.

Weltspiegel 17.02.2021 | Jemen Krieg | Mädchen in Flüchtlingslager
Watoto wakicheza katika kambi ya wakimbizi wa ndani mkoani Marib, Yemen, Februari 16, 2021.Picha: Nabeel al-Awzari/REUTERS

Akielezea kustushwa na kuongezeka kwa mzozo mjini Marib, naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anaseshughulikia masuala ya kibinadamu Mark Lowcock, amesema mashambulizi dhidi ya mji huo yatawaweka hatarini raia milioni mbili, ambapo mamia kwa maelfu wanakabiliwa na uwezekano ya kulaazimika kukimbia.

Shinikizo la kidiplomasia?

Tim Lenderking, mjumbe mpya wa Marekani nchini Yemen aliyeteuliwa na rais Joe Biden kama sehemu ya juhudi za kumaliza vita nchini humo, amewahimiza Wahouthi kusitisha mashambulizi yao.

Lenderking aliwaambia waandishi habari mjini Washington, baada ya ziara katika kanda hiyo, kwamba mashambulizi hayo yanaweza kusababisha ugumu zaidi kwenye miundombinu ya kibinadamu ambayo tayari imeelemewa.

UN Nothilfe Mark Lowcock
Naibu Katibu Mkuu wa UN anaeshughulikia masuala ya kiutu Mark Lowcock.Picha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

"Hatua juu ya Marib siyo mpya. Ni jambo ambalo Wahouthi wamekuwa wakilifikiria kwa muda wa miaka miwili iliyopita. Na iwapo hilo ni kijiweka katika nafasi bora kuelekea majadiliano au nini hasa lengo lao, siwezi kusema," alisema Lenderking.

"Tuna njia za kuwafikishia ujumbe Wahouthi na tunazitumia njia hizo kwa nguvu, kupitia mawasiliano ya moja kwa moja na uongozi wa mataifa muhimu yanayoshiriki."

Soma pia:Miaka 10 tangu vuguvugu la maandamano nchini Yemen

Ripoti za mamia ya vifo pande zote

Maafisa wa kijeshi wanaoiunga mkono serikali waliliambia shirika la habari la AFP kwamba waasi wamesonga mbele kuelekea mji huo kupitia maeneo mawili usiku, baada ya mapigano makali na vikosi vya serikali.

Maafisa hao wamesema wapiganaji kadhaa wameuawa kwa pande zote katika muda wa masaa 24 tu. Idadi jumla ya vifo kutokana na vita vya Marib haijulikani, lakini kuna ripoti zinazozungumzia kuuawa kwa mamia.

Soma pia:Yemen Kusini yachafuka baada ya jaribio la uhuru 

Hadi mwanzoni mwa 2020, mji wa Marib ulikuwa umeepuka hali mbaya kabisa ya mzozo huo wa miaka sita, na uligeuka kimbilio la wengi.

Lakini utulivu huo wa kiasi ulitoweka kufuatia kuongezeka kwa mapigano mwaka uliyopita, na licha ya utulivu kujerea kwa muda mfupi kuanzia Oktoba, hofu inaongezeka juu ya janga jengine la kibinadamu.

Chanzo: Mashirika