1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yasimamisha vikwazo dhidi ya waasi wa Yemen

26 Januari 2021

Utawala wa rais Joe Biden umesimamisha vikwazo vya nchi hiyo dhidi ya kundi la waasi wa Kihuthi nchini Yemen kwa muda wa mwezi mmoja wakati ikitafakari upya hatua ya kuliweka kundi hilo kwenye orodha ya magaidi

https://p.dw.com/p/3oQ1Z
USA Washington | Ansprache Joe Biden bei Online-Vereidigung von Mitarbeitern
Picha: Evan Vucci/Ap Photo/picture alliance

Wizara ya fedha ya Marekani katika ilani yake imesema kuwa shughuli zote na kundi hilo la waasi zitaendelea kuruhusiwa hadi Februari 26. Agizo hilo lililotiwa saini na Bradley Smith, kaimu mkurugenzi wa ofisi ya kudhibiti mali za kigeni, limesema kuwa Marekani haifungulii  pesa zozote ambazo tayari zimelengwa.

Hatua hiyo inakuja baada ya Antony Blinken , chaguo la Biden la waziri wa mambo ya nje kusema kuwa Marekani itafikiria upya mara moja kutajwa kwa kundi hilo la Kihuthi kuwa la kigaidi na kutamatisha usaidizi wa kijeshi kwa operesheni kali ya Saudi Arabia nchini Yemen.

Wakati wa maandamano ya raia wengi nchini Yemen hapo jana, kamanda wa kundi hilo la Kihuthi Brigadia Ahmed Sharaf amesema kuwa walitoka kuandamana dhidi ya uamuzi wa Israeli na Marekani wa kudai kwamba wao ni magaidi ingawa wako katika nyumba zao na kwamba Marekani imetoka ng'ambo kupigana na wao na kuua watoto wao, wanawake na vijana, na kuharibu miundombinu ya Yemen.

Yemen Huthi Kämpfer
Waasi wa Kihuthi nchini YemenPicha: Hani Mohammed/AP Photo/picture-alliance

Wakati huohuo, Umoja wa Ulaya leo umeshtumu uamuzi wa Marekani wa kulitaja kundi hilo la waasi la Kihuthi kama ''magaidi'' na kuonya kuwa hatua hiyo huenda ikatatiza juhudi za amani na kutolewa kwa msaada. Msemaji wa mkuu wa sera za kigeni wa Umoja huo Josep Borrell amesema kuwa uamuzi huo wa Marekani unahatarisha kutatiza juhudi zinazoongozwa na Umoja wa Mataifa za kuafikia suluhisho la kudumu katika mzozo nchini Yemen.

Serikali ya aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump iliyokuwa na ushirikiano wa karibu na Saudi Arabia na upinzani kwa Iran, ililitaja kundi hilo lenye ushirikiano wa Karibu na Iran kama magaidi katika uamuzi ulioanza kutekelezwa Januari 19 - siku moja kabla ya kuapishwa kwa Biden. Aliyekuwa waziri wa mambo ya nje katika serikali ya Trump Mike Pompeo alitangaza hatua hiyo licha ya miezi kadhaa ya onyo kutoka kwa makundi ya misaada kwamba uamuzi huo ungeongeza mateso katika taifa ambapo zaidi ya watu asilimia 80 ya idadi ya watu milioni 29 nchini humo wanahitaji msaada.

Makundi ya msaada wa kibinadamu yanasema kwamba hayana mbadala isipokuwa kushughulika na Wahuthi ambao wanajumuisha serikali katika eneo kubwa la Yemen pamoja na mji mkuu Sanaa.

Maelfu ya watu wamekufa na mamilioni kuhama makazi yao katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka sita nchini Yemen huku Saudia ikipigana kuwaondoa waasi hao na kupendekeza serikali inayotambuliwa kimataifa.