1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSenegal

UN: Hali ya inayoendelea Senegal inatia wasiwasi

13 Februari 2024

Senegal imekata huduma ya mawasiliano ya Intaneti kwenye simu za mkononi na kupiga marufuku maandamano dhidi ya kuahirishwa uchaguzi mkuu, huku Umoja wa Mataifa ukisema unawasiwasi kuhusu namna hali ilivyo nchini humo.

https://p.dw.com/p/4cMIr
Senegal
Serikali Senegal yapiga marufuku maandmano ikisema yatavuruga usafiriPicha: Zohra Bensemra/REUTERS

Huduma hiyo ya mawasiliano ya Intaneti imekatwa kwa mara ya pili mwezi huu, baada ya serikali kuzuwia kufanyika maandamano ya kupinga uamuzi wa Rais Macky Sall wa kuuahirsha uchaguzi mkuu jambo ambalo limeiingiza nchi hiyo katika mgogoro wa kisiasa.

Wizara ya mawasiliano na masuala ya kidijitali ya Senegal, imesema katika taarifa yake kwamba kufuatia kuenea kwa jumbe za chuki katika mitandao ya kijamii ambazo zimekwishachangia maandamano ya vurugu, mawasiliano ya intaneti ya simu za mkononi yamekatizwa kwa muda kuanzia leo tarehe 13 Februari.

Intaneti katika simu za mkononi zilidhibitiwa siku nane zilizopita wakati bunge lilipounga mkono uamuzi wa Sall, kuuahirisha uchaguzi ambao ulikuwa ufanyike Februari 25, ukasogezwa mbele hadi Desemba 15. Uamuzi huo mara moja ulikosolewa na mashirika ya kutetea haki za binaadamu na washirika wakuu wa kimataifa wa Senegal wakiwemo Marekani na Umoja wa Ulaya.

Umoja wa Ulaya waitaka Senegal kutoa hakikisho la uhuru wa kimsingi

Tayari watu watatu wameuwawa na wengine 266 wamekamatwa wakiwemo waandishi habari katika maandamano yaliyofanyika siku ya Ijumaa na Jumamosi kupinga uamuzi huo wa Sall. Liz Throssell, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia haki za binaadamu, amewaambia waandishi habari mjini Geneva kwamba Umoja huo una wasiwasi kufuatia mivutano inayoshuhudiwa katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Throssell amesema kufuatia ripoti za matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji na kudhibitiwa kwa uhuru wa watu na mawasiliano, wanaitolea mwito serikali kuhakikisha inasimamia na kulinda utamaduni wa siku nyingi wa Senegal wa kuheshimu demokrasia na haki za binaadamu.

Ufaransa yataka uchaguzi mkuu kuandaliwa mara moja

Ufaransa | Rais Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Ludovic Marin/REUTERS

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ufaransa, imetoa tamko juu ya mambo yanayoendelea Senegal na kusema ni lazima nchi hiyo iandae uchaguzi mpya haraka iwezekanavyo na kutumia nguvu inayokubalika wakati inapokabiliana na waandamanaji. Wizara hiyo imesema Ufaransa inatoa pole kwa wale waliopoteza maisha wakati wa maandamano ya hivi karibuni.

Mashirika 40 yakiwemo yale ya kiraia, makundi ya kidini na makundi ya wataalamu likiwemo kundi la The Aar Sunu Election yaani "Tuulinde uchaguzi wetu" yalikuwa yameitisha maandamano ya amani leo mjini Dakar, lakini Elymane Haby Kane mmoja ya waandaaji aliliambia shirika la habari la AFP kwamba alipokea barua rasmi kuwa maandamano hayo yamepigwa marufuku kwa sababu yangeweza kuvuruga usafiri. Kane amesema wameyaahirisha maandamano hayo kwa sababu wanataka kuendelea kuheshimu sheria.

Upinzani waungana kupinga kuahirishwa uchaguzi Senegal

Kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu nchini Senegal kunampa nafasi rais wa sasa Macky Sall, kubakia madarakani hadi pale mrithi wake atakapopatikana. Sall amesema alichukua uamuzi huo baada ya mvutano kati ya bunge na baraza la katiba kufuatia kukataliwa kwa wagombea wao.   

Tangazo la kuahirishwa uchaguzi Senegal lazusha kizaazaa

reuters/afp/ap