1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wakusanya dola bilioni 1.2 kuisaidia Yemen

28 Februari 2023

Zaidi ya mataifa 30 yameahidi kutoa msaada wa kibinaadamu wa takriban dola bilioni 1.2 kwa lengo la kuwasaidia raia wa Yemen wanaopitia hali ngumu baada ya miaka minane ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

https://p.dw.com/p/4O479
Martin Griffiths UN Sonderbeauftragter Jemen
Picha: picture-alliance/Keystone/S. Di Nolfi

Mkuu wa Ofisi ya Uratibu wa misaada ya Kiutu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths,  alisema fedha hizo zitasaidia pakubwa kupeleka misaada mwaka huu nchini Yemen, kwa mamilioni ya raia huko wanaokabiliwa na njaa, wakati huu kukiwa na matumaini kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano, huenda yakafungua nafasi ya kupatikana amani ya kudumu.

Umoja wa Mataifa wafadhaishwa na kukosekana fedha za kuisaidia Yemen

Katika Mkutano huo wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva, kiwango cha fedha kilichotolewa cha dola bilioni 1.2 sio kile kilichotarajiwa cha dola bilioni 4.3, lakini Umoja wa Mataifa umesema huenda dola bilioni 2 zikapatikana mwishoni mwa wiki hii katika mkutano huo wa wahisani, wa kuhamasisha utoaji wa msaada kwaajili ya Yemen.

Huu ni mkutano wa saba wa kuisaidia Yemen unaofanyika kila mwaka kwa mwaka wa saba sasa. Umoja wa Mataifa unatumai mkutano ujao utajikita katika kuijenga upya Yemen kuliko kuzungumzia namna raia wa taifa hilo wanavyokufa kwa njaa.

Umoja wa Mataifa watarajia kukusanya dola bilioni 4.27 kwa ajili ya Yemen

Katika Mkutano huo Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken amesema Uchumi wa Yemen pamoja na taasisi zake vimesambaratishwa vibaya kutokana na mgogoro uliopo huku akiahidi msaada wa dolla milioni 444.

Msaada uliotolewa ni wa kibaguzi

Schweiz UN l Jemen-Geberkonferenz in Genf
Baadhi ya raia wa Yemen wakipokea msaada wa kiutu kufuatia taifa leo kukumbwa na mgogoro wa kibinaadamu kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewePicha: Khaled Ziad/AFP

Huku hayo yakiarifiwa Umoja huo unakadiria kuwa zaidi ya watu milioni 21.7 nchini Yemen wanahitaji msaada wa kiutu.

Mkuu wa  Shirika la Kimataifa la Msaada wa Kiutu la Norwegian Refugee Council Erin Hutchinson, amesema dunia imeitelekeza Yemen wakati huu mgumu kwa kutoa robo tu ya kiwango kilichohitajika. Amesema kilichofanyika kinaonesha wazi kwamba baadhi ya watu wanathaminiwa kuliko wengine.

Saudi Arabia na Wahouthi watafuta suluhu Yemen

Hata hivyo Mataifa mengi yalitaka kusitishwa kwa kanuni iliyowekwa na waasi wa Houthi inayowalazimisha wanawake wakiwemo wafanyakazi wa kike wa kutoa misaada kuandamana na walezi wa kiume jambo linalotatiza shughuli za kutoa msaada. Kwa upande wake waziri Mkuu wa Yemen Maeen Abdulmalek Saeed amesema kumaliza janga la kibinaadamu nchini humo kutaanza pale tu vita vitakapokwisha kikamilifu nchini humo.

Yemen imekumbwa na mapigano makali kuanzia mwaka 2014 kati ya waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran na serikali inayotambulika kimataifa inayoungwa mkono na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia.

Mamilioni ya watoto,wanawake hatarini Yemen

Tangu wakati huo vita hivyo vimesababisha maelfu ya vifo na kulifanya taifa hilo kukabiliwa na tatizo kubwa la njaa. Makubaliano ya kusitisha mapigano yalioanza mwezi Aprili mwaka jana yalimalizika mwezi Oktoba, lakini baadhi ya maeneo yamekuwa na utulivu mdogo.

Chanzo: afp