1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamilioni ya watoto,wanawake hatarini Yemen

Hawa Bihoga19 Oktoba 2022

Hali ya njaa imeendelea kutishia uhai wa mamia kwa maelfu ya watoto na wanawake nchini Yemeni, huku kupungua kwa ufadhili wa misaada ya kiutu kunasababisha hali kuwa ni mbaya kutokana na ukosefu wa chakula

https://p.dw.com/p/4IQqv
Jemen Hilfe Katastrophenhilfe Flüchtlinge Flucht
Picha: AHMAD AL-BASHA/AFP/Getty Images

Mapigano yanayoendelea nchini humo kati ya waasi wa Kihouthi na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia yakitanjwa kutishia hali kuwa mbaya zaidi katika taifa hilo maskini zaidi la kiarabu.

Taarifa za mashirika ya misaada ya kiutu kimataifa yameonesha idadi kubwa ya watoto pamoja na wanawake nchini Yemen ipo hatarini kutokana na ukosefu wa chakula

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha takriban watoto milioni 2.2 walio chini ya umri wa miaka 5 wamethiriwa pakubwa.

Taarifa hiyo ya Umoja wa Mataifa inaeleza zaidi, nusu milioni yawatoto wanakabiliwa na utapia mlo mkalihuku wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wapatao 1.3 wakiwa kwenye hali mbaya kutokana na utapia mlo mkali.

Soma zaidi:Hofu ya vita yarejea Yemen kwa kushindwa kurefusha mkataba

Joyce Msuya katibu msaidizi wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa amesema katika ziara yake alioifanya mwezi uliopita nchini humo hali ni ya kusikitisha na msaada wa haraka unahitajika ili kuokoa maisha ya mamia kwa maelfu ya wanawake na watoto.

Hodeida yashuhudia wagonjwa zaidi

Katika mji wa Hodeida ambao una wakaazi takriban milioni tatu, hospitali ya al-Thawra hupokea wagonjwa wapatao 25,000 kila siku wakiwemo watoto wenye utapiamlo mkali.

Jemen | Unterernährtes Kind
Mkono wa mtoto anaepata matibabu ya utapiamloPicha: Mohammed Mohammed/Photoshot/picture alliance

Nabouta Hassan, daktari katika hospitali hiyo amewaambia waandishi wa habari kwamba kuzorota kwa afya ya watoto hutokea kutokana na vita vinavyoleta ugumu wa watu kupata matibabu.

"Watoto hao wanakabiliwa na utapiamlo unaofikia hatua ya viungo vyao kushindwa kufanya kazi kabisa."

Alisema daktari na kuongeza kwamba utapiamlo ni ugonjwa ambao unaotokea sababu ya kupuuzwa.

"Kuzorota kwa afya ya watoto hutokana na vita na ugumu wa watu kupata hospitali na madaktari walio mbali." Alisema daktari huo

Ripoti za kimataifa msaada wa haraka unahitajika

Kwa mujibu wa shirika la kimataifa la Save the Children, kila dakika kumi nchini Yemen mtoto mmoja hufariki kutokana na maradhi yanayoweza kuzuilika.

Iran yasema mashambulizi ya Houthi dhidi ya Saudia ni onyo

Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa limepunguza mgao wa chakula kwa mamilioni ya watu kutokana na kupungua kwa ufadhili na kupanda kwa bei za chakula duniani.

Shirika hilo limeweka kipaumbele kwa watu milioni 13.5 nchini humo ambao wapo kwenye hatari zaidi.

Umoja wa Mataifa umesema kwamba mwishoni mwa mwezi Septemba  ufadhili kwa ajili ya kukabiliana na hali ngumu nchini Yemen ulifikia dola bilioni 2 kati ya dola bilioni 4.27 zilizohitajika kutoa misaada ya kiutu ili kuokoa maisha ya watu milioni 17.9

Vita nchini Yemen vimeendelea kwa miaka minane kati ya waasi wa Houth na vikosi vinavyoungwa mkono na serikali vinavyopata ushirika kutoka muungano wa mataifa ya Kiarabu ya Kisunni.

Soma zaidi:Je,Yemen itaunda makubaliano mapya?

Tangu wakati huo zaidi ya watu 150,000 wameuwawa kufuatia ghasia hizo na wengine milioni 3 waliyahama makaazi yao.

Theluthi mbili ya watu wanapata chakula cha msaada.Ingawaje kunamakubaliano, hadi hivi sasa pande zote za mzozo zimeshindwa kurefusha makubaliano hayo kwa mara nyingine mwezi huu.