1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa mataifa, New York. Annan kukabiliwa na shutuma za mwanawe kuhusika katika kashfa ya mpango wa mafuta kwa chakula nchini Iraq.

28 Machi 2005
https://p.dw.com/p/CFSm

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Kofi Annan anakabiliwa na hali zaidi ya fadhaa wakati ripoti mpya juu ya mpango wa umoja wa mataifa ya mafuta kwa ajili ya chakula nchini Iraq itakapomlenga mtoto wake wa kiume Kojo kutokana na shughuli zake za kibiashara katika mpango huo.

Uchunguzi huo uliokuwa chini ya uongozi wa kiongozi wa zamani wa benki kutoka Marekani Paul Volcker utatoa shutuma kwa Bwana Annan kwa kushindwa kutambua mgongano wa kimaslahi kwa kuipa kazi kampuni ambayo mwanae anafanyakazi katika mpango huo. Bwana Annan pamoja na umoja wa mataifa wamekuwa wakihusishwa na kashfa hiyo ya mafuta kwa ajili ya chakula nchini Iraq, mpango wa umoja wa mataifa ambao ulikuwa ukiangalia mauzo ya mafuta katika utawala wa Sadam Hussein nchini Iraq kuazia mwaka 1996 hadi 2003, kwa kununulia mahitaji ya kiutu.