1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu wamuaga Malkia Elizabeth II

Hawa Bihoga
19 Septemba 2022

Viongozi wa ulimwengu wamekusanyika kwenye kanisa la kale la Westminster Abbey mjini London kuhudhuria ibada ya mazishi ya Malkia Elizabeth wa II aliyeaga dunia kiasi wiki mbili zilizopita akiwa na umri wa miaka 96.

https://p.dw.com/p/4H3Cy
Queen Eilzabeth II, Staatsbegräbnis
Picha: Stephen Lock/i Images/IMAGO

Ulimwengu unaungana na Uingereza leo Jumatatu katika mazishi ya kitaifa ya Malkia Elizabeth II, ambapo marais, Wafalme, mawaziri wakuu wa mataifa mbalimbali pamoja nawatu takriban milioni moja wakiwa kandokandoya barabara za mji wa London kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho kwa Malkia huyo ambae alikalia kiti cha enzi kwa kipindi cha miaka 70.

Siku ya leo Jumatatu imetangazwa kama siku ya mapumziko kwa umma ikiwa ni kumuenzi Malkia Elizabeth II ambae alifariki Septemba 8 akiwa na umri wa miaka 96.

Mazishi hayo yataoneshwa moja kwa moja na mataifa takriban 200 ulimwenguni kote, kadhalika maafisa wa polisi watakuwa katika oparesheni muhimu katika kile kinachoonekana kuimarisha hali ya usalama.

Soma pia:Viongozi wa ulimwengu waanza kukusanyika nchini Uingereza kwa ajili ya kuhudhuria mazishi ya Malkia Elizabeth wa ll.

Kabla ya mazishi ya kiongozi huyo aliohudumu kwa kipindi kirefu zaidi, Mfalme Charles III alitoa ujumbe wa shukrani kwa watu nchini Uingereza na dunia kwa ujumla wake akisema yeye na mkewe Camilla wamefarijika kutokana na idadi kubwa ya watu ambao wamejitokeza kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho kwa Malkia.

"Wakati tunapojiandaa kutoa heshima zetu za mwisho,nachukua fursa hii kusema ahsante kwa watu wote wasioweza kuhesabika ambao wamekuwa faraja na msaada kwa familia yangu na mimi mwenyewe katika kipindi hiki cha majonzi" Alisema Mfalme Charles III

Katika mazishi, jeneza la Malkia Elizabeth litabebw  kutoka ukumbi wa Westminster, ng'ambo ya barabara kuelekea Westminster Abbey, kwenye gari la kifalme, gari ambalo lilitumika kubeba majeneza ya viongozi wengine wa taifa hilo akiwemo Edward VII, George V na George VI, pamoja na aliekuwa waziri mkuu wa zamani wa taifa hilo Winston Churchill.

Eneo la ibada ya mazishi

Katika ibada itakayofanyika Gothic medieval abbey sehemu ambayo Malkia Elizabeth alifunga ndoa na mume wake mwanamfalme Philip mwaka 1947 na kutawazwa mwaka 1953 itahudhuriwa na watu takriban 2000 wakiwa ni pamoja na viongozi wa dunia, wahudumu wa afya na pamoja na makundi mengine.

Großbritannien | Staatsbegräbnis Queen Elizabeth II
Waombolezaji wakiwa katika ibada ya maziko ya Malkia Elizabeth IIPicha: Frank Augstein/AFP/Getty Images

Hata hivyo mamlaka ya mji wa London imesema maeneo yote ya umma ambayo jeneza la Malkia litapita tayari yamefurika watu kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho.

Rais wa Marekani Joe Biden na mkewe Jill wamewasili huko Westminster Abbey kwa ajili mazishi ya kitaifa ya Malkia Elizabeth II.

Kiongozi huyo wa Marekani ni miongoni mwa mamia ya wakuu wa nchi na viongozi wa kisiasa kutoka sehemu mbalimbali duniani wakihudhuria ibada ya mazishi huko mjini London.

Soma pia:Mwili wa Malkia Elizabeth II wawasili ukumbi wa Westminster

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na William Ruto wa Kenya ni miongoni mwa wakuu wa nchi wanashiriki ibada hiyo itakayofuatiwa na mazishi ya kitaifa baadae leo katika Karsi la Windsor.

Jeneza la Malkia Elizabeth II tayari limeondoka katika ukumbi wa bunge wa Westminster likiwa limebebwa na askari kuelekea kwenye mazishi ya kitaifa ambayo yatafanyika faraghani.

Jeneza hilo liliwekwa katika ukumbi huo tangu siku ya ya Jumatano na kutoa fursa kwa mamia kwa maelfu ya waombolezaji kutoa heshima zao za mwisho kwa Malkia huyo.

Nchini Ujerumani bendera kwenye majengo ya umma zinapepea nusu mlingoti leo Jumatatu ikiwa ni kuungana na waingereza katika wakati huu mgumu wa mazishi ya kitaifa ya Malkia wao Elizabeth II yanayofanyika mjini London.

Malkia wa Uingereza anazikwa leo