1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu uko kwenye njia panda asema Volker Turk

Idhaa ya Kiswahili9 Septemba 2024

Mkuu wa Tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ameonya kwamba ulimwengu unahitaji kubadilisha njia ili kuepuka mustakabali uliojaa migogoro ya kijeshi.

https://p.dw.com/p/4kQwc
Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa awalaumu wanasiasa wanaojaribu kudidimiza uhuru wa kujieleza
Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa awalaumu wanasiasa wanaojaribu kudidimiza uhuru wa kujieleza Picha: Salvatore Di Holfi/KEYSTONE/picture alliance

Akifungua kikao cha Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa huko Geneva, Volker Turk alisisitiza kuwa ulimwengu uko kwenye njia panda. Kwa hiyo kunahitajika hatua za haraka.

"Tunaweza kuendelea na hali yetu ya sasa, ambayo ni hali mpya ya hila, na siku za usoni zenye kiza, au tunaweza kuamka na kubadilisha mambo kwa ubora, kwa ubinadamu na kwa ajili ya sayari. Hali mpya ya kawaida haiwezi kukomeshwa. Hali ya kuongezeka wasiwasi wa kijeshi na njia za kiteknolojia zinazozidi kutisha, udhibiti na ukandamizaji. Hali mpya ya kutojali kwa kuongezeka kwa usawa ndani na nje ya nchi.", alisema Turk.

Kabla ya kuongeza : "Dunia haitakiwi kuwa eneo huru la usambazaji taarifa potofu, ukweli unaofifisha, na kubana uwezo wa kufanya maamuzi huru na yenye ufahamu."

Akizungumzia vita huko Mashariki ya kati, Ukraine na Sudan, Turk alisisitiza kwamba nchi hazipaswi na haziwezi kukubali kupuuzwa kwa wazi kwa sheria za kimataifa. Mkuu wa Tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa amesema hali hii lazima ishughulikiwe kikamilifu.

Israel yaamuru raia kuondoka kaskazini mwa Gaza

Wakaazi wa Gaza kaskazini watakiwa kuondoka makwao
Wakaazi wa Gaza kaskazini watakiwa kuondoka makwaoPicha: Bashar Taleb/AFP

Hotuba hiyo ya Turk imetolewa huku Israel ikiamuru kuahamishwa tena kwa baadhi ya watu wa maeneo ya kaskazini mwa ukanda wa Gaza. Israel imesema wanamgambo wa Palestina wametumia maeneo hayo kurusha makombora kwenye mji wake Ashkelon.

Hayo yamejiri huku mwaka mpya wa shule katika maeneo ya Palestina ukianza rasmi leo Jumatatu, pamoja na kwamba shule zote za Gaza zimefungwa baada ya miezi 11 ya vita. Hadi kufikia sasa juhudi zote za kidiplomasia za kusitisha vita bado hazijafanikiwa.

Takriban asilimia tisini ya wakazi wa Gaza wameyakimbia makaazi yao, wengine wamehamishwa mara kadhaa kutoka eneo moja kwenda jengin. Mamia ya maelfu ya watu wamejazana kwenye kambi za mahema kando ya pwani ya ukanda huo, huku wengi wakikosa huduma za msingi.

Shambulizi la roketi lauwa watu 12 katika milima ya Golan

Mashambulizi ya anga Syria

Wizara ya afya huko Gaza inayoendeshwa na Hamas ilisema leo Jumatatu kwamba takriban watu 40,988 wameuawa katika vita kati ya Israel na wanamgambo wa Palestina, ambavyo sasa vinaingia mwezi wake wa 12.

Usiku wa kuamkia leo, Israel ilifanya mashambulizi ya anga nchini Syria. Taasisi ya uchunguzi wa vita vya Syria, iliripoti vifo vya watu 18 wakiwemo wapiganaji wanane. Taasisi hiyo imesema mashambulizi hayo yayilenga kituo cha utafiti wa kisayansi huko Masyaf, katika mkoa wa Hama na maeneo mengine na kuharibu majengo na vituo vya kijeshi.