1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine:Hatuhusiki na hujuma dhidi ya mabomba ya gesi

Hawa Bihoga
8 Machi 2023

Waziri wa ulinzi wa Ukraine Oleksii Reznikov amesema serikali ya nchi yake haikuhusika na hujuma dhidi ya mabomba yanayosafirisha gesi kutoka Urusi kwenda Ujerumani, kufuatia ripoti ya uchunguzi .

https://p.dw.com/p/4OPPZ
Frankreich Ukrainischer Verteidigungsminister Resnikow in Frankreich
Picha: JULIE SEBADELHA/REUTERS

Uchunguzi uliofanywa na mashirika ya utangazaji ya umma ya Ujerumani ya ARD na SWR pamoja na gazeti la Die Zeit uliihusisha Ukraine na milipuko ya mwezi Septemba 2022 kwenyemabomba mawili ya kusafirisha gesi kati ya Urusi na Ujerumani.

Maafisa nchini Ujerumani, Sweden, Denmark, Uholanzi na Marekani walihusika na uchunguzi, limeripoti gazeti la Die Zeit. Kwa mujibu wa vyombo vya habari, ikiwemo gazeti la New York Times, wachunguzi mpaka sasa hawajapata ushahidi wa nani aliamuru hujuma hiyo.

Vikiwanukuu maafisa mbalimbali ambao hawakutajwa majina, vyombo hivyo vya habari viliripoti kwamba wanaume watano na mwanamke walitumia boti iliyokodishwa na kampuni inayomilikiwa na raia wa Ukraine aishiye nchini Poland kufanya shambulio hilo.

Soma zaidi:Marekani: Mripuko wa mabomba ya Nord Stream ilikua hujuma

Gazeti la New York Times liliripoti pia Jumanne kwamba maafisa wa Marekani walipitia taarifa za ujasusi zilizoashiria kuwa kundi linaloiunga mkono Ukraine ndilo lililohusika na milipuko hiyo. Lakini waziri wa ulinzi wa Ukraine, Oleksiy Reznikov, amekana kuhusika kwa serikali.
Kwangu mimi, ni hadithi ya kushangaza kidogo" alisema na kuongeza kwamba taarifa hiyo haihusiki chcochote na Ukraine.

 Aliongeza kuwa "nadhani uchunguzi wa mamlaka rasmi utaelezea kwa undani."

 Pistorius:Tusubiri ripoti rasmi ya uchunguzi

Akizumgumza kwenye mkutano wa waandishi habari mjini Stockholm, waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius, amezungumzia juu ya ripoti hiyo.

Schweden | EU Verteidigungsministertreffen | Boris Pistorius
Waziri wa ulinzi Ujerumani Boris PistoriusPicha: Frandsen/EUC/ROPI/picture alliance

Amesema baadhi ya wataalamu wamezungumzia pia uwezekano kwamba shambulizi hilo lilikuwa operesheni ya uongo iliyofanywa na kundi linalojifanya kuwa la Waukraine.

Soma zaidi:Scholz, Biden waahidi kuendelea kuisaidia Ukraine

Amesema lengo la mpango huo ni kuiharibia sifa Ukraine, na kuongeza kuwa hii haitokuwa mara ya kwanza katika historia ya matukio kama hayo.
"Nasita kutoa tathmini ya  wazi kuhusu utafiti huo." Alisema

Ameongeza kwamba kilicho muhimu zaidi, kwa sasa ni NATOna nchi zinazozunguka Bahari ya Baltic, bahari ya kaskazini,kulinda usalama.

"Tuje pamoja na kufanya kila kitu kulinda miundombinu yetu muhimu katika bahari." Alisisitiza

Urusi yaishutumu Marekani dhidi ya shambulizi hilo

Msemaji wa Baraza la Usalama la Taifa la Ikulu ya White House John Kirby alikataa jana kuzungumzia ripoti ya New York Times,akibainisha kuwa uchunguzi wa Denmark, Ujerumani na Sweden bado unaendelea.

Soma zaidi:Guterres alaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov Jumatano hii amezitaja ripoti hizo kuwa ghiliba iliyoratibiwa yenye nia ya kuwaficha wapangaji halisi wa shambulio hilo.

Rais wa Urusi Vladimir Putin na maafisa wake wameituhumu Marekani kupanga milipuko hiyo, ambayo waliielezea kama shambulio la kigaidi.

Urusi yaendelea kushambulia miji ya Ukraine kwa makombora