1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ukraine yataja masharti ya kufanya mazungumzo na Moscow

Sylvia Mwehozi
8 Novemba 2022

Ukraine imeshikilia msimamo wake mkali juu ya uwezekano wa mazungumzo na Urusi ikisema kwamba majadiliano yanaweza kufanyika endapo tu Moscow itakuwa tayari kuyerejesha maeneo yote ya nchi hiyo inayoyadhibiti.

https://p.dw.com/p/4JCtu
Ukraine | Präsident Wolodymyr Selenskyj
Picha: Ukrainian President'S Office/APA Images/ZUMA/picture alliance

Matamshi hayo yametolewa siku chache baada ya vyombo vya habari vya Marekani kuripoti kwamba Washington imeihimiza Kyiv kuonyesha utayari wa mazungumzo wakati ambapo uchaguzi wa bunge wa katikati mwa muhula nchini Marekani ukitarajiwa kutoa hatma ya uungwaji mkono wa mataifa ya Magharibi kwa Ukraine.

Katika hotuba yake kabla ya kuhutubia viongozi wa ulimwengu katika mkutano wa kilele wa mazingira, Rais Volodymyr Zelenskiy alisema Urusi lazima isukumwe katika mazungumzo "ya kweli", akiorodhesha masharti ya kufanyika kwa mazungumzo hayo ya kusaka amani.Ikulu ya Kremlin yakataa kuthibitisha mazungumzo na Marekani

Miongoni mwa matakwa yaliyotolewa na Zelensky ni pamoja na kurejeshwa kwa maeneo ya Ukraine yanayodhibitiwa na Urusi, fidia kwa uharibifu uliosababishwa na vita, sambamba na kuwashitaki wahusika kwa kile alichosema ni "uhalifu wa kivita."

Ukraine Armee rückt weiter vor
Wanajeshi wa Ukraine mkoani DonetskPicha: Anatolii Stepanov/AFP/Getty Images

Zelensky ameongeza kuwa Ukraine imewahi mara kwa mara kupendekeza mazungumzo kama hayo lakini wamekuwa wakipokea kile alichokiita "majibu ya wendawazimu" kutoka Urusi pamoja na mashambulizi ya kigaidi na makombora.

Tangu Urusi ilipotangaza kuyatwaa maeneo ya Ukraine mwishoni mwa Septemba, Zelensky aliweka bayana kwamba Kyiv haitokaa kwenye mazungumzo na Moscow kama Vladimir Putin ataendelea kuwa rais. Maafisa wa Kyiv wamerejelea matamshi hayo katika siku za hivi karibuni, wakisisitiza kwamba watakuwa tayari kuketi chini na mrithi wa Putin.

Katika mahojiano na gazeti la Italia la Repubblica yaliyochapishwa siku ya Jumanne, mshauri wa Rais Zelensky, Mykhailo Podolyak, amenukuliwa akisema kwamba "kujadiliana na Putin kutamaanisha kushindwa na hatuwezi kumpatia zawadi hiyo".

Russland | Sitzung Sicherheitsrat | Wladimir Putin
Rais Vladimir Putibn wa UrusiPicha: Sergei Ilyin/SPUTNIK/AFP/Getty Images

Katibu wa baraza la usalama la Ukraine Oleksiy Danilov, naye ameandika kupitia Twitter akisema kwamba kurejeshwa kwa mipaka ya Ukraine ndio sharti la awali la mazungumzo na kwamba Kyiv inahitaji hakikisho la mifumo ya kisasa ya ulinzi wa anga, ndege za kivita, mizinga na makombora ya masafa marefu.

Siku ya Jumatatu, msemaji wa Ikulu ya Urusi ya Kremlin Dmitry Peskov alirejelea msimamo wa Moscow kwamba iko tayari kwa mazungumzo lakini ni Kyiv ambayo imekuwa ikikataa. Moscow imesema mara kwa mara haitajadiliana juu ya maeneo ambayo inadai imeyanyakua kutoka Ukraine.

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi Andrei Rudenko amesisitiza siku ya Jumannne kwamba Urusi haitoi masharti yoyote juu ya kuanza kwa mazungumzo na kuituhumu Kiev kwa kukosa "dhamira ya dhati". "Haya ni maamuzi yao, siku zote tumeonyesha utayari wa mazungumzo kama hayo", alisema Rudenko.

Vikosi vya Ukraine vimekuwa kwenye mashambulizi hivi karibuni, wakati Urusi ikijipanga tena kutetea maeneo ya Ukraine ambayo bado inayadhibiti. Urusi imekuwa ikiwahamisha raia kutoka maeneo inayoyakalia haswa mji wa kusini wa Kherson, katika operesheni ambayo Ukraine inadai kuwa ni ya lazima.

Urusi kwa upande wake inasema kwamba inawahamisha raia katika maeneo salama.