1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano makali yatarajiwa Kherson

26 Oktoba 2022

Afisa mmoja mwandamizi wa Ukraine amesema Urusi inajiandaa kwa "mojawapo ya mapambano makali" katika eneo la kimkakati la Kherson lililoko kusini mwa Ukraine.

https://p.dw.com/p/4IhDp
Ukraine-Krieg - Nowa Kachowka
Picha: AP/dpa/picture alliance

Haya yanafanyika wakati ambapo Urusi inajiandaa kuutetea mji mkubwa ulio chini ya udhibiti wake nchini humo.

Wanajeshi wa Urusi katika wiki za hivi karibuni wamesukumwa nyumana mashambulizi ya Ukraine na wako katika hatari ya kunaswa katika ukingo wa magharibi wa mto Dnipro, eneo ambalo ndilo makao makuu ya jimbo la Kherson ambalo limekuwa likidhibitiwa na Urusi tangu siku za mwanzo za uvamizi wa Ukraine, miezi minane iliyopita.

Maafisa wa mamlaka iliyowekwa na Urusi nchini humo wamekuwa wakiwataka wakaazi wa eneo hilo kukimbilia ukingo wa mashariki wa mto Dnipro ila mshauri wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, Oleksiy Arestovych, amesema hakuna dalili za majeshi ya Urusi yenyewe kujiandaa kuuacha mji huo.

Ukraine Krieg | Zivilisten werden aus Cherson evakuiert
Raia waliookolewa kutoka mji wa Kherson wakielekea CrimeaPicha: Alexander Ermochenko/REUTERS

Urusi yaishitaki Ukraine Umoja wa Mataifa

Rais Zelenskiy amerudia kutoa ahadi yake ya kulirudisha katika udhibiti wa Ukraine eneo la Kherson na iwapo hilo litafanyika basi itakuwa ni pigo kubwa mno kwa Rais Vladimir Putin wa Urusi.

"Nawashukuru wote wanaotusaidia kupigania uhuru. Namshukuru kila mmoja anayepigania ushindi wetu. Nawashukuru wanajeshi wetu wote ambao kwa sasa wanapambana na waliokalia ardhi yetu kimabavu na kuipa Ukraine kilicho muhimu kwake ambacho ni imani katika mustakabali wetu," alisema Zelenskiy.

Wakati huo huo Urusi imeishitaki Ukraine kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikisema inajiandaa kutumia bomu la nyuklia.

Ila Ukraine inasema inahofia kwamba madai hayo ni ishara kwamba Urusi hasa ndiyo inayojiandaa kutumia mabomu hayo katika operesheni yake.

USA, New York | Dmitry Polyanskiy stellvertretender UN-Botschafter von Russland
Dmitry Polyansky, balozi wa Uris katika Umoja wa MataifaPicha: John Lamparski/NurPhoto/picture alliance

Papa Francis awataka wanasiasa kukomesha vitisho vya nyuklia

Rais wa Marekani Joe Biden amesema Urusi itakuwa inafanya kosa kubwa iwapo itatumia bomu la nyuklia katika mashambulizi yake inayoyafanya.

Naye kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amewaongoza viongoziwa dini tofauti duniani katika wito wa kuwataka wanasiasa kuzuia kitisho cha matumizi ya silaha za nyuklia katika vita vya Ukraine.

Wakati hayo yakiarifiwa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya imezitaka nchi na makampuni katika umoja huo kuchangisha fedha na vifaa ili kuisaidia sekta ya nishati nchini Ukraine, ambayo zaidi ya thuluthi moja imeharibiwa na maroketi yaliyorushwa na Urusi.

Chanzo: Reuters/AP