1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine: Wito wa Urusi wa kusitisha mapigano ni mtego.

6 Januari 2023

Ukraine imelipinga pendekezo la rais wa Urusi Vladimir Putin la kusimamisha mapigano kwa muda kwa ajili ya sherehe za Krismasi kwa Waorthodox. Imeserma hatua hiyo ni hila tu za Urusi.

https://p.dw.com/p/4Lnqx
Ukraine Russische Soldaten
Picha: Konstantin Mihalchevskiy/SNA/IMAGO

Urusi imetoa wito wa kusitishwa mapigano kuanzia saa 6 mchana kwa saa za huko mnamo Januari 6 hadi saa sita usiku Januari 7 kwa ajili ya kuadhimisha sherehe za Krismasi kwa waumini wa madhehebu ya Orthodox lakini rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema pendekezo hilo la Urusi la kusitisha vita kwa muda kwa ajili ya Krismasi kwa waumini wa madhehebu ya Orthodox ni njama za Urusi za kuzuia kasi ya Ukraine ya kufikisha vifaa vya kijeshi na kusonga mbele majeshi ya nchi hiyo kwenye maeneo muhimu yanayokabiliwa na vita. 

Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky na mkewe Olena Zelensky.
Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky na mkewe Olena Zelensky.Picha: AFP

 

Rais wa Urusi, Vladimir Putin ameyaagiza majeshi yake kusimamisha mapigano kwa muda wa saa 36 kuanzia mchana wa leo tarehe 6 hadi hapo kesho usiku tarehe 7 ili kuruhusu sherehe za krismasi za za waumini wa madhehebu ya Orthodox. Sherehe hizo za krismasi huadhimishwa wakati huu na nchi zote mbili za Urusi na Ukraine.

Kwa mujibu wa taarifa, Putin ametoa pendekezo hilo baada ya kiongozi mkuu wa kanisa la Orthodox la Urusi askofu Kirill mwenye umri wa miaka 76 kutoa mwito ili kuwawezesha waumini kusherehekea siku kuu ya Krimasi. Kulingana na ikulu ya Urusi hii ni mara ya kwanza kwa nchi hiyo kutangaza usitishaji kamili wa mapigano nchini Ukraine tangu ilipoanzisha mashambulizi mwezi Februari mwaka jana.

Soma:Putin: Urusi iko tayari kwa mazungumzo.

Mshauri wa rais wa Ukraine Mykhailo Podolyak ameandika kwenye ukurasa wake waTwitter kwamba "Urusi ni lazima iondoke katika maeneo ya Ukraine inayoyakalia hapo ndipo maafikiano ya muda yatakapoanzia vinginevyo ibaki tu na unafiki wake."

Naye rais Zelensky amesema majeshi ya Ukraine yanasonga mbele hasa wakati huu ambapo viongozi wa Marekani na Ujerumani wametangaza kwamba wataipa nchi hiyo magari ya kivita kwa ajili ya kuyaongezea nguvu majeshi yake.

Soma:Ukraine kupokea magari zaidi ya kivita

Rais wa Marekani Joe Biden na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz walikubaliana siku ya Alhamisi kupeleka nchini Ukraine magari hayo ya kijeshi pamoja na silaha nyingine katika hatua inayoashiria kwamba nchi za magharibi zinatekeleza azimio lao jipya la kuongeza msaada wa kijeshi kwa Ukraine kwa lengo la kuuzima uvamizi wa Urusi.

Kushoto: Rais wa Marekani Joe Biden. Kulia: Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz.
Kushoto: Rais wa Marekani Joe Biden. Kulia: Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz.Picha: Jonathan Ernst/REUTERS

Ujerumani pia imesema itafanya kama Marekani kwa kupeleka mfumo wa kisasa wa makombora nchini Ukraine ili kuisaidia kuzuia mashambulizi ya anga ya Urusi. Viongozi hao wawili wamesema Marekani na Ujerumani vilevile zitatoa mafunzo kwa wanajeshi wa Ukraine. Kwenye taarifa ya pamoja Biden na Scholz wamesisitiza tena mshikamano wao usioyumba na nchi ya Ukraine na watu wake katika kukabiliana na uchokozi wa Urusi.

Agizo la Putin la kusitisha mapigano kwa muda amelitoa siku moja baada ya Urusi kutangaza kuongezeka kwa idadi ya vifo na kufikia watu 89 baada ya mashambulio mabaya zaidi yaliyofanywa na Ukraine dhidi ya Urusi.

Vyanzo:AFP/AP