1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yapuuzia miito ya kuitisha uchaguzi

Sylvia Mwehozi
10 Juni 2024

Serikali ya Ujerumani imetupilia mbali miito ya kuitaka iitishe uchaguzi wa mapema kufuatia kuanguka kwa vyama vinavyounda muungano tawala katika uchaguzi wa bunge la Ulaya.

https://p.dw.com/p/4gscj
Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani (katikati) akiwa na mawaziri wa serikali yake
Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani(katikati) akiwa na mawaziri wa serikali yakePicha: TOBIAS SCHWARZ/AFP/Getty Images

Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Hebestreit amenukuliwa hii leo mjini Berlin akisema kuwa uchaguzi wa Ujerumani utafanyika mwaka ujao wakati wa majira ya machipuko kulingana na ratiba ya kawaida.

Soma:Ujerumani: Wafuasi wa chama kipya cha siasa BSW waipinga AFD

Ameendelea kueleza kuwa "hakuna wakati,  hata kwa sekunde" ambapo kumekuwa na wazo la kwamba Ujerumani inaweza kuitisha uchaguzi mpya kwa sasa. Ameongeza kuwa muungano wa serikali ya Scholz ni mradi wa miaka minne na kwamba utakapomalizika, wapiga kura watakuwa na usemi kwa mara nyingine.

Kauli hizo zinatolewa baada ya vyama vitatu katika muungano tawala wa Kansela Olaf Scholz, vyote kwa pamoja kupata chini ya theluthi moja ya kura, huku chama cha Social Democrats cha SPD kikishuhudia matokeo mabaya zaidi katika uchaguzi wa taifa, hali iliyozusha maswali kuhusu mustakabali wa serikali yake. Kumekuwa na miito kutoka kwa chama cha kihafidhina cha upinzani cha CDU, miongoni mwa vyama vingine vinavyotaka kura ya kutokuwa na imani na Kansela Scholz katika bunge na uchaguzi mpya wa bunge.

Uchaguzi wa bunge la Ulaya | DW ikizungumza na mbunge wa bunge la Ulaya David McAllister kutoka kundi la vyama vya kihafidhina
DW ikizungumza na mbunge wa bunge la Ulaya David McAllister kutoka kundi la vyama vya kihafidhinaPicha: DW

Fuatilia:  Vyama vya kihafidhina vyashikilia viti vingi bunge la Ulaya

Profesa mmoja wa sayansi ya siasa kutoka shule ya Hertie, Andrea Römmele amesema kuanguka kwa muungano wa Scholz sio suala la kushangaza kwasababu raia wa Ujerumani hawaiungi mkono serikali kwa sasa.

"Ukitazama uchaguzi wa Ulaya mara zote unachukuliwa kama kanuni ya uchaguzi wa pili, ambako raia ni kama wanazipigia kura serikali za kitaifa. Na hali ilivyo Ujerumani ni kwamba watu wanapinga serikali kwasasa. Kwahiyo si kitu cha kushangaza. Lakini kiwango cha namna walivyoanguka ndio kinashutua kuhusu muungano huo tawala."

Soma: Uchaguzi wa Bunge la Ulaya kudhoofisha muungano wa Scholz?

Katika hatua nyingine chama cha siasa kali za mrengo wa kulia ama kikijulikana kama chama mbadala kwa Ujerumani cha AfD, kimetangaza kumwondoa mgombea Maximilian Krah kutoka katika ujumbe wa chama hicho ndani ya Bunge la Ulaya. Ujumbe wa AfD ndani ya bunge hilo sasa utaongozwa na Rene Aust aliyechaguliwa na wajumbe wa chama hicho siku ya Jumatatu. Mwanasiasa Rene Aust ni naibu kiongozi wa AfD katika jimbo la Thuringia.

Tino Chrupalla | Alice Weidel | AfD
Viongozi wa AfD Tino Chrupalla na Alice WeidelPicha: Annegret Hilse/REUTERS

Kiongozi mwenza wa AfD Alice Weidel ametangaza uamuzi huo mapema siku ya Jumatatu huko Berlin, saa chache baada ya matokeo ya uchaguzi kuonyesha kuwa chama hicho kimeongeza viti vingi na kuibuka nafasi ya pili kitaifa kwa asilimia takribani 16 ya kura.

Krah amekuwa mgombea anayeongooza wa AfD katika uchaguzi wa Ulaya uliomalizika, lakini alizuiwa kufanya kampeni na chama hicho kuelekea uchaguzi. Mwanasiasa huyo amegubikwa na kashfa kadhaa, ikiwemo madai ya kwamba alipokea hongo kutoka Urusi na China.