1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muungano wa Scholz kupoteza nguvu uchaguzi wa bunge la Ulaya

9 Juni 2024

Baada ya miaka miwili na nusu serikalini, muungano wa siasa za wastani za mrengo wa kushoto wa Kansela Olaf Scholz unatarajiwa kupoteza nguvu zake katika uchaguzi wa bunge la Ulaya uliofanyika leo kote nchini humo.

https://p.dw.com/p/4gqWC
Uchaguzi wa bunge la Ulaya | Kansela Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akipiga kura yake katika uchaguzi wa bunge la Ulaya katika kituo cha kupigia kura Potsdam, Ujerumani 09 06 2024. Picha: Janine Schmitz/photothek/IMAGO

Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Alternative für Deustchland - AFD yaani Mbadala kwa Ujerumani kinagombea kuwa cha pili chenye nguvu, kwa mujibu wa utafiti wa maoni.

Leo ndio siku ya mwisho ya uchaguzi unaofanyika kote barani Ulaya ambao ulianza Alhamisi na unafanyika katika mataifa 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Uchaguzi huo wa Umoja wa Ulaya unaonekana kuwa mtihani kwa uongozi wa Scholz ikiwa ni miezi kadhaa kabla ya uchaguzi katika majimbo kadhaa mwezi Septemba.

Soma pia: Wapiga kura wahitimisha uchaguzi wa bunge la Ulaya 

Ujerumani ambalo ni taifa kubwa kabisa kiuchumi barani Ulaya, itatoa viti 96 kati ya 720 katika Bunge la Umoja wa Ulaya. Vita nchini Ukraine, uhamiaji, na athari za sera ya mabadiliko ya tabianchi kwa wakulima ni miongoni mwa maswala yaliyopo kwenye fikra za wapiga kura.

Uchunguzi unaashiria kuwa vyama vikuu na vinavyounga mkono sera za Ulaya vitabakia na wingi wao wa viti bungeni, lakini vitapoteza viti kwa vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia kama vile vinavyoongozwa na Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni, Kiongozi wa Hungary Viktor Orban, Geert Wilders wa Uholanzi na Marine Le Pen nchini Ufaransa.