Ujerumani yatoa wito wa kuliimarisha shirika la afya duniani
13 Aprili 2020Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema hayo katika tahariri aliyoandika kwenye gazeti la "Welt am Sonntag”. Waziri Maas amesema Ujerumani inadhamiria kwa uthabiti wote kupambana na janga la maambukizi ya virusi vya corona na pia ametoa mwito wa kuliimarisha shirika la afya duniani WHO. Maas amesisitiza juu ya juhudi za kupatikana chanjo dhidi ya COVID-19.
Ujerumani imeahidi kutekeleza uongozi imara ili kuzisaidia nchi nyingine za Umoja wa Ulaya katika juhudi za kukabiliana na maambukizi ya corona na kulishinda janga hilo. Katika muda huo wa kuwa Rais wa Umoja wa Ulaya, Ujerumani itakuwa na wajibu wa kuongoza vikao vya baraza la Umoja wa Ulaya na kushauri ajenda za baraza la jumuiya hiyo.
Waziri Maas ameeleza kuwa majukumu ya kwanza yatakayotekelezwa na Ujerumani ni kulegeza vizuizi vya kudhibiti usafiri na vizuizi vya masoko ya ndani. Ameeleza kuwa hayo yatafanyika hatua kwa hatua kwa kushauriana na wote
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani pia ametanabahisha kwamba mpaka sasa hakuna chanjo na wala tiba dhidi ya COVID-19 na kwa hivyo kinachohitajika ni mshikamano, badala ya kutupiana lawama. Amesema mshikamano ni muhimu katika juhudi za kulishinda janga la corona. Amesisitiza kwamba ikiwa viongozi wa Umoja wa Ulaya watajifunza kutokana na janga la corona, jumuiya yao itaibuka na nguvu zaidi na nchi zao zitaungana zaidi kuliko hapo awali.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas pia ametoa mwito wa ushirikiano mkubwa katika upatikanaji na uzalishaji vifaa vya kuokolea uhai na wakati huo huo kuendeleza ugavi wa mahitaji na kuboresha njia za kuwakinga raia.
Katika tahariri yake waziri Maas amewakosoa wale wanaolitumia janga la corona kwa shabaha za kisiasa, amesema watu hao wanakiuka demokrasia na utawala wa kisheria. Amesema kuweka vizuizi kwa kisingizio cha kudhibiti maambikizi ya corona ni jambo lisilokubalika. Katika muktadha huo waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani alikuwa anazungumzia juu ya hatua zilizochukuliwa nchini Hungary. Ameoanya kwamba yeyote anayekiuka maadili ya msingi ya Umoja wa Ulaya asitarajie kunufaika kikamilifu na misaada ya fedha ya jumuiya hiyo.
Bwana Maas amesema Ujerumani inataka kuliona bara ya Ulaya lenye afya na kuona uchumi wa dunia unaofanya kazi ili kuiwezesha Ujerumani kuendeleza shughuli za mauzo ya nje vilevile amefafanua kwamba msaada wa Euro biloni 500 kwa ajili ya nchi za Umoja wa Ulaya ambao ni mkubwa kabisa katika historia ya Umoja huo siyo tu ni ishara ya mshikamano bali pia ni kwa ajili ya sababu za kiuchumi ambazo ni muhimu sana kwa Ujerumani.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesisitiza katika tahariri yake kwamba jambo muhimu kabisa katika vita vya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona ni kuimarisha kazi za Umoja wa Mataifa na shirika lake la afya WHO hasa katika juhudi za kuzalisha na kugawa vifaa vya kufanyia vipimo na kupatikana kwa chanjo na ametilia maanani kuliimarisha shirika hilo ambalo kwa sasa halipatiwi fedha za kutosha.
Chanzo/DW
Mhariri: Sudi Mnette