1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania

Florence Majani11 Aprili 2022

Waziri wa Nchi katika Wizara ya Mambo ya Nje wa Ujerumani yuko nchini Tanzania kwa ziara ya siku tatu,kujadili masuala kadhaa ya uhusiano kati ya Tanzania na Ujerumani.

https://p.dw.com/p/49mV3
Tansania Die Präsidentn von Tansania Samia Suluhu Hassan mit der Staatsminsterin des Auswärtigenamtes Katja Keul
Picha: Tanzania Statehouse

Waziri Katja Keul amesema ziara yake inalenga kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi yake na Tanzania wakati huu muhimu ambapo dunia inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo vita vinavyoendelea katikati mwa Ulaya kufuatia uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine:

''Nimefurahi kuwa hapa, ingawa tuna nyakati ngumu, kwa kuwa tuna vita Ulaya  hata hivyo ni fursa nzuri kwetu kuendelea kuimarisha uhusiano huu kati ya Ulaya na Afrika  na uhusiano wetu huu ni wa karibu na wa muhimu  kuliko wakati mwingine wowote, kwa sababu wote tupo katika mtumbwi mmoja, hivyo hii  ni safari muhimu kwetu'' alisema Keul

Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kutembelewa na Waziri Keul baada ya Mali, tangu serikali mpya ya muungano wa vyama vitatu vya SPD, Kijani na FDP ilipoingia madarakani Desemba mwaka jana. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock pia anazuru bara la Afrika wiki hii.

Soma pia→Ujerumani yaisaidia Tanzania kupambana na COVID-19

Mikataba 3 baina ya Ujerumani na Tanzania

Waziri wa Nchi kwenye wizara ya Mambo ya Je wa Ujerumani, Katja Keul  akisindikizwa na balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Regine Hess wakutana na Rais Samia Suluhu
Waziri wa Nchi kwenye wizara ya Mambo ya Je wa Ujerumani, Katja Keul akisindikizwa na balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Regine Hess wakutana na Rais Samia SuluhuPicha: Tanzania Statehouse

Hapo jana Waziri Keul alishuhudia utiaji saini wa mikataba mitatu, wa kwanza ni ukarabati wa jengo la kihistoria, ambapo makumbusho ya kwanza ilipowekwa mwaka 1939 na mkataba wa pili ni utafiti na onyesho la pamoja, utakaongazia turathi za kimila na kihistoria zilizochukuliwa Tanzania na kupelekwa Ujerumani, kabla ya kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa upinzani na mkataba wa kuendesha programu mbalimbali za kuelimisha jamii kupitia semina na mikutano kwa kushirikiaana na Wajerumani. 

Waziri Keul amesifu juhudi za serikali ya Tanzania za kutunza mazingira na bioanuwai na kusema nchi yake inataka kujifunza kutokana na uzoefu wa Tanzania.

''Kama nilivyosikia kuhgusu Tanzania, inafanya vizuri katika utunzaji wa bioanuai, kwa kulinda asilimia 30 ya ardhi na hiyo ni hatua nzuri na muhimu na sisi tunajitahidi sana kutoa ushirikiano  kwa kadri tuwezavyo katika hilo, kuhakikisha kwamba mabadiliko ya tabia nchi, hayawaathiri wale ambao hawajayasababisha. Tunatakiwa kuwajibika'',alisema Katja Keul.

Soma pia →Ujerumani yaisaidia Afrika Mashariki katika mambo muhimu

Katika mikataba hiyo ya mashirikiano Serikali ya Ujerumani itatoa jumla ya Euro 201,130 kwa ajili ya kusaidia katika ukarabati wa jengo la King George V lililopo Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni jijini Dar es Salaam na kuandaa onesho la historia ya Tanzania kwa pamoja ambalo litawekwa mjini Berlin Ujerumani na  baadaye Tanzania.

Waziri Keul amekutana pia na wanafamilia ya Mangimeli kuzungumzia mchakato wa kurejesha mabaki yake yaliyochukuliwa na utawala wa kikoloni wa Ujerumani.