1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kufunga kabisa shughuli wakati wa pasaka

23 Machi 2021

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametangaza kuongeza muda wa vizuizi vya kufunga shughuli hadi Aprili 18. Merkel ameonya ni lazima Ujerumani izuie kuongezeka kwa wimbi la tatu la maambukizi.

https://p.dw.com/p/3qz5W
Deutschland | Nach Beratungen von Bund und Ländern | Bundeskanzlerin Angela Merkel | Pressekonferenz
Picha: Michael Kappeler/REUTERS

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametangaza leo kuongeza muda wa vizuizi vya kufunga shughuli hadi Aprili 18. Merkel ameonya ni lazima Ujerumani izuie kuongezeka kwa wimbi la tatu la maambukizi, katika wakati ambapo idadi ya visa imefikia viwango ambavyo maafisa wanasema vitapelekea vyumba vya wagonjwa mahututi kuelemewa. 

Maafisa wamesema Ujerumani itaingia kwenye hatua kali zaidi ya kufunga shughuli katika kipindi cha sikukuu za pasaka kuanzia Aprili Mosi hadi 5. Katika kipindi hicho maduka makubwa ya bidhaa yatafunguliwa siku ya Jumamosi tu inayoangukia katikati ya tarehe hizo, ambayo ni tarehe 3.

Mazungumzo ya makubaliano kuhusu hatua hizo kali baina ya mawaziri wakuu wa majimbo yote 16 ya Ujerumani na kansela Angela Merkel yalidumu hadi masaa ya alfajiri leo kutokana na mjadala mkali ulioibuka mara kwa mara.

Awali, maafisa wa afya walionya wimbi la tatu la maambukizi limepindukia kiwango cha juu, na mamlaka zina wasiwasi vyumba vya wagonjwa mahututi vitaelemewa. Tangazo hili la sasa linabatilisha lile la awali ambapo vizuizi hivyo vilikuwa vinafikia ukomo Machi 28.

Ni hatua gani mpya?

Katika kipindi hicho cha siku tano, makanisa yataruhusiwa kuendesha ibada za pasaka kwa njia ya mtandao. Idadi ya watu wanaotakiwa kukutana kutoka kwenye familia mbili tofauti haitazidi watano katika kipindi hicho hicho. Vituo vya chanjo vitabakia wazi. Mikusanyiko itazuiwa, maduka karibia yote yatafungwa.

Merkel amesemaje?

Deutschland | Nach Beratungen von Bund und Ländern | Bundeskanzlerin Angela Merkel | Pressekonferenz
Kansela Merkel(katikati) amesema Ujerumani inakabiliwa na hali mbaya kwa sasaPicha: Michael Kappeler/REUTERS

Kansela Angela Merkel alinukuliwa akisema Ujerumani inakabiliwa na hali mbaya sana kutokana na kuenea kwa virusi vinavojibadilisha vya corona. Aliuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba kwa sasa taifa hilo linakimbizana na muda ili kuhakikisha linawachanja watu wake na katika kipindi hiki hakuna namna nyingine zaidi ya kuanzisha upya hatua hizi kali.

"Katika kipindi hiki cha siku tano kutakuwa na zuio la mikusanyika ya umma, kula maeneo ya wazi, ambayo awali yaliruhusiwa na maduka ya vyakula tu yataruhusiwa kufunguliwa siku ya Jumamosi. Pia tutawasiliana na jumuiya za kidini kuwaomba wafanye ibada kwa njia ya mtandao katika kipindi hiki. Na ninasisitiza, hili ni ombi!"

Amesema iwapo Ujerumani haitafanikiwa kuvikabili virusi hivyo, ni wazi kwamba vizuizi havitaondolewa.

Viongozi wa majimbo wanasemaje?

Waziri mkuu wa Bavaria Markus Söder aliwaambia waandishi wa habari kwamba nia hasa ya vikwazo hivyo ni kuhakikisha wanaviondoa kwa haraka virusi hivyo vipya. Alisema, ni wazi kwamba watu wanaishi kwenye awamu hatari kabisa ya janga la corona, na kuongeza kuwa wengi wanadharau mazingira yaliyopo.

Deutschland | Coronavirus - Beratungen von Bund und Ländern - Pressekonferenz
Wakuu wa maimbo wanakubaliana na hatua hizo ili kupambana na viruis hivyo vipyaPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Gavana wa Berlin Michael Müller amesema ni muhimu kuhakikisha watu wanautumia muda huo vizuri hadi pale chanjo itakapowafikia.

Iwapo kutatokea eneo linakabiliwa na maambukizi ya watu 100 kati ya 100,000 kwa siku tatu mfululizo, kutatangazwa hatua kali zaidi na Idadi ya watu kukutana itapunguzwa hata zaidi.

Mapema jana Jumatatu naibu msemaji wa serikali Martina Fietz alisema kiwango cha maambukizi kimeongezeka kwa kiasi kikuwa, na virusi vya corona vinavyojibadilisha ambavyo kwa mara ya kwanza viligundulika Uingereza hivi sasa vimejikita nchini Ujerumani.

Hatua hizi zitaathiri vipi safari?

BG Corona-November in Deutschland | Lufthansa startet Antigen-Schnelltests
Wasafiri wanaorejea Ujerumani watatakiwa kupima kabla ya kuingia nchini humoPicha: Sven Hoppe/dpa/picture alliance

Wasafiri wanaorejea kutoka nje watatakiwa kujiweka karantini na kuhakikisha hawana maambukizi ya corona baada ya kupimwa kabla ya kurejea Ujerumani.

Maafisa awali waliwaomba waajiri kuwapatia waajiriwa wao ambao hawawezi kufanyia kazi nyumbani angalau kipimo kimoja cha COVID-19 kinachotoa majibu ya haraka kila wiki ama baada ya wiki mbili iwapo vitapatikana.

Makubaliano ya mwisho yalikuwaje?

Katika mkutano wao wa mwisho mapema mwezi huu, viongozi hao walikubaliana kuanza kufungua maduka lakini kwa tahadhari, licha ya kitisho cha aina mpya ya virusi.

Chini ya makubaliano hayo, wabunge walikubaliana kuanza kwa hatua kufungua maduka ya rejareja, saluni na bustani ili kuruhusu watu kukutana tena baada ya kuzuiwa kwa zaidi ya miezi minne.

Kufungwa kabisa shughuli "hakutasaidia."

Hata hivyo, msemaji wa kamati ya afya ya bunge la Ujerumani Profesa Andrew Ullman hata hivyo ameiambia DW kwamba hatua hiyo ya kufunga kabisa shughuli haitasaidia kwa kuwa hii si mara ya kwanza na tayari jamii imechoshwa nayo.

Idadi ya visa vilivyothibitishwa vya maambukizi hadi jana Jumatatu iliongezeka na kufikia milioni 2,667,225 na vifo vikifikia 74,714.

Mashirika: DW