1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza kufanyia kazi mpango wa kuzalisha mazao imara

20 Novemba 2023

Sunak anatarajiwa kutangaza mpango wa kisayansi wa kuzalisha mazao yanayostahamili athari za mabadiliko ya tabia nchi katika wakati ambapo serikali yake inaanda kongamano la kimataifa la usalama wa chakula mjini London.

https://p.dw.com/p/4Z9lk
Uingereza | Rishi Sunak
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi SunakPicha: Kin Cheung/REUTERS

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak anatarajiwa kutangaza mpango wa kisayansi wa kuzalisha mazao yanayostahamili athari za mabadiliko ya tabia nchi, katika wakati ambapo serikali yake inaanda kongamano la kimataifa la usalama wa chakula mjini London kuanzia leo Jumatatu.

Kongamano hilo, ambalo ni ushirikiano kati ya Uingereza, Somalia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Mfuko wa uwekezaji wa watoto CIFF na Wakfu wa Bill na Melinda Gates, linatarajiwa kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka zaidi ya mataifa 20.

Sunak ameeleza umuhimu wa kushughulikia changamoto za uhaba wa chakula duniani.

Uingereza imesema mpango huo wa kisayansi utaongozwa na muungano wa taasisi za utafiti wa kilimo CGIAR ambao pia utashirikiana na wanasayansi wa Uingereza ili kuzalisha mazao yanayostahamili athari za mabadiliko ya tabia nchi na magonjwa sugu.

Serikali ya Uingereza imesema pia inatoa msaada wa kibinadamu wa hadi pauni milioni 100 kwa nchi zinazokabiliwa na uhaba wa chakula ikiwemo Ethiopia, Sudan, Sudan Kusini na Afghanistan, na pia kwa nchi zilizoathirika na majanga ya kiasili kama vile Malawi.