1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

Uganda yaadhimisha siku ya mazingira Duniani

5 Juni 2023

Kila Juni 5, dunia huadhimisha Siku ya Mazingira na kaulimbiu ya mwaka huu ni kupambana dhidi ya uchafuzi unaotokana na matumizi ya plasitiki.

https://p.dw.com/p/4SDGU
Äthiopien Einwohner in Dire Dawa sammeln gebrauchte Kunststoffe zum Recyceln.
Picha: Mesay Mekonnen/DW

Hii ni baada ya kubainika kuwa ni asilimia 10 tu ya plastiki inayozalishwa duniani ndiyo hutumika tena na iliyobaki huchafua mazingira kwa namna mbalimbali pamoja na kuathiri afya za watu. Vita dhidi ya uchafuzi ni wajibu wa kila binadamu.

Kulingana na takwimu za mashirika mbalimbali ya kimataifa, zaidi ya tani milioni 400 ya plastiki huzalishwa kila mwaka duniani, huku kiasi kikubwa cha plastiki hii ikibaki ardhini, hadi asilimia 23 yake huishia mitoni, kwenye maziwa na bahari na inapochomwa, moshi wake hutishia maisha ya watu na viumbe hai moja kwa moja. Plastiki ndogondogo hupatikana katika vyakula, maji na hewa kutokana na sumu. 

Naye Shadrach Nirere ambaye ni mwanaharakati wa mazingira aliyeanzisha kikundi cha vijana wanaopambana dhidi ya uchafuzi wa plastiki nchini Uganda.

Hata hivyo, kuna mikakati na juhudi za kukabiliana na uchafuzi unaotokana na matumizi ya plastiki kupitia mbinu mbalimbali za kisayansi. Kwa mfano nchini Uganda, wenye viwanda ambao wanakosolewa kuwa vyanzo vya uchafuzi wa plastiki wameanza kuwekeza katika ukusanyaji wa taka hiyo na kuitumia tena kama malighafi.

Juhudi za Afrika Mashariki

Äthiopien Einwohner in Dire Dawa sammeln gebrauchte Kunststoffe zum Recyceln.
Picha: Mesay Mekonnen/DW

Juhudi sawa na hizi zinashuhudiwa katika mataifa mengine ya Afrika Mashariki. Mojawapo ya miradi ijulikanayo kama ''taka ni mali'' inayofadhiliwa kwa kiasi fulani na shirika la maendeleo la Ujerumani, GIZ, imezinduliwa na Baraza la Wafanyabiashara Afrika Mashariki, EABC. Ijapokuwa Shadrach anapongeza juhudi hizi anatahadharisha kuwa bado kuna safari ndefu kufanikisha jitihada hizo kupunguza uchafuzi unaotokana na matumizi ya plastiki.

Huku sera na sheria za kudhibiti na kupiga marufuku matumizi ya plastiki zikizaa matunda katika baadhi ya nchi kama Uganda, kuna tatizo kubwa katika utekelezaji wake jaribio la kupiga marufuku plastiki hasa mifuko ya kufungasha maarufu kama kaveeera halijazaa matunda Uganda.

Wadau wanahimiza viwanda kuwajali zaidi ya watu milioni 20 duniani wanaojishughulisha na kukusanya taka za plastiki kama njia ya wao kujiingizia kipato. Jumuiya hiyo ni ya watu masikini wanaotegemea kipato kutokana na taka hizo na kuchangia pakubwa katika kupambana na mienendo ya uchafuzi unaotokana na matumizi ya plastiki.