1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yataka machafuko ya Tibet yakome

Charo,Josephat26 Machi 2008

Rais Sarkozy asema yuko tayari kuongoza mazungumzo

https://p.dw.com/p/DTen
Rais wa Ufaransa Nicolas SarkozyPicha: picture-alliance/ dpa

Ufaransa leo imetoa mwito machafuko ya Tibet yakome. Sherehe ya kuwasha mwenge wa michezo ya Olimpiki imetatizwa kwa muda mfupi mjini Olympia nchini Ugiriki hii leo wakati watu walipojaribu kufanya maandamano ya kuipinga China.

Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, amemtaka rais wa China, Hu Jintao, na serikali ya mjini Beijing ijizuie katika kuyamaliza machafuko ya Tibet. Rais Sarkozy anataka mazungumzo ya haraka yafanyike kati ya maafisa wa China na wafuasi wa kiongozi wa kidini, Dalai Lama na kusema Ufaransa itakuwa tayari kuongoza mazungumzo ya kuumaliza mgogoro wa Tibet.

Katika ujumbe wake rais Sarkozy ameeleza huzuni yake kufuatia matukio ya kuhuzunisha yaliyotokea hivi majuzi huko Tibet.

Ujumbe huo umetumwa baada ya majuma mawili ya maandamano dhidi ya utawala wa China huko Tibet, ambayo kwa mujibu wa viongozi wa Tibet wanaoishi uhamishoni, yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 130. Ujumbe huo umetumwa pia wakati kukiwa na miito ya kutaka michezo ya Olimpiki igomewe.

Mwishoni mwa juma lililopita, Pierre Moscovici, kiongozi wa chama cha kisoshalisti, alimshutumu rais Sarkozy kwa kunyamaa kimya kuhusu hali huko Tibet na kumtaka atoe matamshi makali dhidi ya China.

Mgomo dhidi ya Olimpiki

Kura mpya ya maoni iliyofanywa nchini Ufaransa inaonyesha Wafaransa wengi wanamtaka rais Sarkozy aigomee sherehe ya ufunguzi wa michezo ya Olimpiki itakayofanyika mwezi Agosti mwaka huu mjini Beijing, kwa sababu ya hali mbaya ya haki za binadamu nchini China.

Kamati ya Olimpiki ya hapa Ujerumani leo imetangaza kuwa imepitisha uamuzi wa kupinga kuigomea michezo ya Olimpiki nchini China, lakini hata hivyo imeelezea wasiwasi wake kuhusu machafuko yanayoikabili Tibet na maeneo jirani.

Mwenge umewashwa

Serikali ya Ugiriki leo imelaani hatua ya watetezi watatu wa haki za binadamu raia wa Ufaransa kuitatiza kwa muda mfupi sherehe ya kuuwasha mwenge wa michezo ya Olimpiki mjini Olympia nchini Ugiriki. Katika sherehe ya kuadhimisha kuanza kwa safari ya miezi mitano ya mwenge wa Olimpiki, iliyoonyeshwa moja kwa moja ulimwenguni kote, mchezaji filamu Maria Nafpliotou, ameuwasha mwenge huo mbele ya hekalu ya Hera.

Entzündung des Olympischen Feuers
Mwenge wa michezo ya Olimpiki ukiwashwa mjini Olimpia UgirikiPicha: picture-alliance/ dpa

Hata hivyo kabla kuuwasha, waandamanaji watatu walifaulu kuwapita maafisa wa polisi wakiwa wamebeba bango jeusi likiwa na pingu tano mfano wa pete tano za nembo ya Olimpiki. Walimkaribia kiongozi wa kamati ya China inayoandaa michezo ya mjini Beijing, Liu Qi, wakati alipokuwa akiwahutubia mamia ya maafisa, lakini wakakamatwa na kuondolewa na polisi. Duru za polisi zinasema watu hao wanazuiliwa na watashitakiwa kwa kuvuruga amani.

Shirika la waandishi wa habari wasio na mipaka limesema watu hao watatu ni wanachama wake waliojaribu kufanya maandamano hayo. Linasema serikali ya China haipaswi kuuchukua mwenge wa Olimpiki ambao ni ishara ya amani, pasipo kulaani hali ya haki za binadamu nchini humo. Katibu mkuu wa shirika hilo, Robert Menard, alilifunua bango la pili alipokuwa ameketi katika eneo la viongozi mashuhuri na baadaye akakamatwa.

China inamlaumu Dalai Lama kwa kuwa na njama ya kuivuruga michezo ya Olimpiki kwa kuandaa maandamano huko Tibet.

Lawama

Hii leo, binamu wa Dalai Lama, ambaye ni mbunge wa Tibet anayeishi uhamishoni, Khedroob Thondup, ameishutumu China kwa kuyakandamiza maandamano ya Tibet akitaja hatua hiyo kuwa uvamizi wa tatu wa serikali ya Beijing wa eneo hilo.

Indien Tibet China Dalai Lama in Neu Delhi
Dalai LamaPicha: AP

Khedroob Thondup amesema uvamizi wa kwanza ilikuwa hatua ya China kuikalia kijeshi Tibet kuanzia mwaka wa 1950 hadi 1959 na wa pili ulikuwa kuzindua reli inayotoka Beijing kwenda Lhasa mnamo mwaka jana.

Amesema China inaogopa kumruhusu Dalai Lama arejee Tibet kwa kuwa Watibet wengi wanampenda na kusisitiza kwamba mtu anayeweza kuyamaliza machafuko ya Tibet ni Dalai Lama.

Maandamano dhidi ya China

Wakati haya yakiarifiwa, polisi nchini Nepal wamewatawanya wakimbizi na watawa wa kibudha 200 wa Tibet waliokuwa wakiandamana karibu na ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Kathmandu hii leo. Polisi wamewatandika waandamanaji hao kutumia fimbo za mianzi na kuwatia mbaroni watu 40. Waandamanaji hao wanautaka Umoja wa Mataifa uchunguze ukandamazaji wa maandano ya Tibet uliofanywa na maafisa wa China.

Wakipiga kelele za kuitaka China ikomeshe mauaji ya Watibet, waandamanaji hao walitembea kwenda katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Kathmandu wakati polisi walipowasimamisha yapata mita 100 kabla kuyafikia makao hayo na kuwapokonya mabango waliyokuwa wameyabeba.