1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani: Wagombea wajibizana kuhusu uchumi

17 Februari 2025

Wagombea wakuu wanne wa ukansela nchini Ujerumani Friedrich Merz, Olaf Scholz, Robert Habeck, na Alice Weidel, wamefanya mdahalo wa moja kwa moja wa televisheni jana Jumapili, wiki moja kabla ya zoezi la kupiga kura.

https://p.dw.com/p/4qaCD
Ujerumani 2025 | Mdahalo wa Televisheni kati ya Scholz, Habeck, Merz na Weidel kuhusu Uchaguzi wa Bundestag
Kansela Olaf Scholz (SPD), Waziri Robert Habeck (Die Grünen), Friedrich Merz (CDU), na Alice Weidel (AfD) wakishiriki mdahalo wa televisheni kuhusu kampeni ya uchaguzi wa Bundestag.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Zikiwa zimesalia siku saba tu kabla ya uchaguzi mkuu wa Ujerumani, vyama vya upinzani vya mrengo wa kulia vinaendelea kuongoza kwenye kura za maoni.

Chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union (CDU) kinachoongozwa na Friedrich Merz kinaungwa mkono kwa takriban asilimia 30, huku chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, Alternative for Germany (AfD) cha Alice Weidel, kikiwa na asilimia 20.

Chama cha Social Democratic (SPD) cha Kansela Olaf Scholz, cha mrengo wa kati-kushoto, kinashika nafasi ya tatu kwa asilimia 15, huku mshirika wao katika serikali ya mseto, chama cha Kijani kinachoongozwa na Robert Habeck, kikiwa nafasi ya nne kwa zaidi ya asilimia 13. 

Wafuasi wa Merz
Wafuasi wanaoumuunga mkono mgombea wa CDU Friedrich MerzPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Soma pia:Wagombea Ukansela wa Ujerumani wachuana kwenye mdahalo

Katika mdahalo wa televisheni uliofanyika Jumapili, wagombea walijadili kwa kina masuala ya uchumi wa Ujerumani pamoja na msimamo wao kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Merz na Scholz walimkosoa Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, kwa kile walichokiita kuingilia siasa za Ujerumani baada ya hotuba yake kwenye Mkutano wa Usalama wa Munich siku ya Jumamosi.

Kwa upande wake, Weidel, aliyekutana na makamu huyo wa rais pembezoni mwa mkutano huo, alisisitiza umuhimu wa kuwa na uhusiano mzuri na utawala wa Donald Trump. 

Msimamo kuhusu Ukraine

Wagombea wote wanne walielezea uungaji wao mkono kwa Ukraine, huku Weidel wa AfD akishutumiwa kwa kuwa na msimamo wa kuegemea Urusi.

Friedrich Merz, mgombea wa CDU/CSU, alisema kuwa Rais wa Urusi Vladimir Putin anaangazia ardhi ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO kama shabaha yake kuu.

 Rais Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: John Thys/AFP

Aliongeza kuwa vita vya Urusi sio tu dhidi ya Ukraine, bali dhidi ya mfumo mzima wa kisiasa ulioundwa mwaka 1990. Merz pia alimkosoa Weidel kwa kushindwa kumlaumu Putin kwa uvamizi huo. 

Hata hivyo, Weidel alitetea msimamo wa chama chake, akisema:  "Ujerumani ingependeza zaidi kuwa mpatanishi asiyeegemea upande wowote katika utatuzi wa migogoro ya kimataifa.

Soma pia:Scholz na Merz wapambana kwa maneno bungeni

Tunataka kuleta amani. Tunataka usitishaji wa mapigano nchini Ukraine. Na tunamshukuru Mungu kwamba sasa Donald Trump yuko madarakani, ambaye pia anataka hilo."

Siku chache baada ya mazungumzo ya simu kati ya Putin na Rais wa Marekani Donald Trump, ambayo yalionekana kufungua njia kwa mazungumzo ya amani kuhusu Ukraine, Kansela Olaf Scholz alisisitiza kuwa hakuna mtu yeyote anayeweza kuamua mustakabali wa Waukraine bila wao kushirikishwa moja kwa moja. 

Makamu Kansela Robert Habeck wa chama cha Kijani alionya kuwa utawala wa Trump umeanzisha "mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya maadili ya jamii ya Magharibi" na kusisitiza kuwa, "hatupaswi kwa hali yoyote kujidhalilisha mbele ya Marekani kwa matamko haya."

Sera ya uhamiaji

Mdahalo huo haukuishia kwenye masuala ya uchumi na Ukraine pekee, bali pia uligusia sera ya uhamiaji.

Wagombea walionyesha tofauti kubwa katika mitazamo yao kuhusu jinsi ya kushughulikia ongezeko la wahamiaji nchini Ujerumani, suala ambalo limekuwa mjadala mkali katika kampeni hizi za uchaguzi. 

Ujerumani yaelemewa na mzigo wa wahamiaji

Soma pia:Wabunge wa Ujerumani kupigia kura muswada tata wa uhamiaji

Kwa kuwa uchaguzi huu unatarajiwa kuwa na matokeo yenye athari kubwa kwa Ujerumani na Ulaya kwa ujumla, mdahalo huo umeibua hisia kali miongoni mwa wapiga kura.

Itasalia kuonekana ikiwa Merz na CDU wataendeleza uongozi wao kwenye kura za maoni hadi siku ya uchaguzi au ikiwa vyama vya mseto wa sasa vitaweza kurudisha uungwaji mkono wao.