Ujerumani: Wagombea Ukansela wachuana kwenye mdahalo
17 Februari 2025Wagombea hao walijadili mada muhimu kuhusu Ujerumani na masuala ya kimataifa.
Olaf Scholz, Friedrich Merz, Robert Habeck na Alice Weidel, walishindana kwa hoja kuhusu sera ya uhamiaji, vita vya Ukraine na mdororo wa uchumi ikiwa imesalia karibu wiki moja tu kabla ya uchaguzi mkuu wa kitaifa.
Kansela wa sasa wa Ujerumani Olaf Scholz aliitetea rekodi ya utawala wake kufuatia ukosoaji wa mpinzani wake wa kihafidhina Friedrich Merz, ambaye kura za maoni zinaupa kipaumbele muungano wa chama chake cha CDU na CSUkwa asilimia 30.
Licha ya majibizano makali, kulishuhudiwa pia katika mdahalo huo kauli zinazoashiria umoja kati ya Scholz, Merz na Habeck hasa katika suala la kuendeleza msaada kwa Ukraine na kukosoa kauli za viongozi wa Marekani kuhusu demokrasia ya Ulaya na mazungumzo yajayo ya amani katika mzozo wa Ukraine.