1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mrengo wa kushoto washinda uchaguzi wa bunge France

7 Julai 2024

Muungano wa vyama vya mrengo wa kushoto ulioundwa kabla ya uchaguzi wa mapema wa France umeshinda viti vingi zaidi katika duru ya pili huku chama cha mrengo mkali wa kulia cha National Rally kikiambulia nafasi ya tatu.

https://p.dw.com/p/4hzMf
Uchaguzi wa bunge nchini Ufaransa
Kiongozi wa Muungano wa New Popular Front, NFP, Jean-Luc Melenchon amesifu mafanikio ya kihistoria ya muungano wake. Picha: Arnaud Journois/dpa/MAXPPP/picture alliance

Muungano wa vyama vya mrengo wa kushoto wa New Popular Front, NFP umepata ushindi wa kushtukiza dhidi ya chama cha mrengo wa kulia cha National Rally (RN) katika duru ya pili ya uchaguzi wa bunge wa 2024 nchini Ufaransa. Hakuna muungano, hata hivyo, umeweza kupata wingi wa kujitosheleza kuunda serikali kivyake.

Ukosefu wa wingi kwa muungano wowote unatishia kuitumbukiza Ufaransa katika msukosuko wa kisiasa na kiuchumi. Matokeo ya mwisho hayatarajiwi hadi Jumapili jioni au mapema Jumatatu katika uchaguzi huo wa mapema, ambao uliitishwa wiki nne tu zilizopita katika kile ambacho wadadisi walikitaja kama kamari kubwa ya Macron.

Soma pia: Wafaransa wapiga kura duru ya pili ya uchaguzi wa Bunge

Ni kamari ambayo haionekani kuwa imemlipa rais huyo alieshuka umaarufu, ambaye muungano wake umepoteza udhibiti wa bunge, kulingana na makadirio. Chama cha mrengo mkali wa kulia cha National Rally, chake Marine Le Pen kimeongeza pakubwa  idadi ya viti vyake, wakati huo huo, lakini kimeshuka sana kwenye matarajio yake.

Uchaguzi wa Bunge Ufaransa
Wafuasi wa chama cha France Unbowed wakisherehekea kwenye makao makuu ya chama hicho mjini Paris, Jumapili usiku, Julai 7, 2024, baada ya matokeo kuonyesha muungano wao umeshinda viti vingi zaidi.Picha: Thomas Padilla/AP/picture alliance

NFP: tuko tayari kutawala

Kiongozi wa muungano wa NFP Jean-Luc Mélenchon amemtaka Macron kuualika muungano huo kuunda serikali, kutokana na makadirio ambayo yanauweka katika uongozi. Muungano huo, alisema, "uko tayari kutawala."

Katika uwamba wa Stalingrad mjini Paris, wafuasi wa mrengo wa kushoto walishangilia na kupiga makofi huku matokeo ya awali yalionyesha kwenye skrini yakionyesha muungano huo ulikuwa mbele.

Vifijo na shangwe pia vilisikika katika uwanja wa Republique plaza mashariki mwa Paris, huku watu wakiwakumbatia watu wasiowafahamu na dakika kadhaa za makofi bila kukoma baada ya matokea ya kwanza kutangazwa.

Soma pia: Jukumu la Macron katika Umoja wa Ulaya huenda likadhoofishwa na duru ya pili ya uchaguzi

Muungano wa New Popular Front unatazamiwa kuwa na viti 172-215, huku muungano wa Rais wa Emmanuel Macron wa Ensemble ukiwa katika nafasi ya pili kwa wabunge 150 hadi 180. Chama cha Marine Le Pen kimemaliza kwa mshangao katika nafasi ya tatu kwa viti 120 hadi 152.

Macron ashinda awamu ya pili ya urais

Bunge lisilo na chama chenye wingi wa wazi linaweza kuzitumbukiza siasa za Ufaransa katika machafuko kwa wiki kadhaa za mashauriano kuamua nani atahudumu kama waziri mkuu. Macron anaweza kulaazimika kuongoza nchi sambamba na waziri mkuu anaepinga sehemu kubwa ya sera zake za mrengo wa kati.

Matokeo hayo yatashawishi msimamo wa Ufaransa kueleka vita vya Ukraine, diplomasia ya kimtaifa na utulivu wa kiuchumi wa Ulaya. Ofisi ya Macron ilisema rais huyo "atasubiri bunge jipya lijipange" kabla ya kufanya maamuzi yoyote.

National Rally chalia na Macron

Katika hotuba yake baada ya kura, Jordan Bardella, rais wa chama cha National Rally, alishutumu hila za kisiasa ambazo zilipelekea chama hicho kutofikia matarajio na kumlaumu Macron kwa "kuitumbukiza Ufaransa katika hali ya mashaka na ukosefu wa utulivu."

Idadi isiyo na kifani ya wagombea waliofuzu duru ya pili ilijiweka kando ili kuruhusu mgombea wa upinzani kuchuana na na mgombea wa National Rally, na hivyo kuongeza nafasi ya kuwashinda wagombea hao wa mrengo mkali wa kulia.

Soma pia: Vyama vya siasa kuungana Ufaransa kukizuia chama cha Le Pen?

"Usiku wa leo, kwa kuchukua jukumu la kudhoofisha taasisi zetu kimakusudi, Emmanuel Macron ... anawanyima Wafaransa majibu yoyote ya matatizo yao ya kila siku kwa miezi mingi ijayo," Bardella alisema.

Uchaguzi wa Bunge Ufaransa 2024 | Paris | Jordan Bardella
Rais wa chama cha National Rally Jordan Bardella amemlaumu Rais Macron kwa kuitumbukiza Ufaransa katika mashaka ya kisiasa Picha: Sarah Meyssonnier/REUTERS

Tofauti na mataifa mengine barani Ulaya ambayo yamezoea zaidi serikali za mseto, Ufaransa haina utamaduni wa wabunge kutoka kambi pinzani za kisiasa kuja pamoja kuunda miungano ya wingi.

Muda ambao Ufaransa imetumbukia katika mashaka ya kisiasa umekuwa mbaya sana, mnamo wakati michezo ya kimataifa ya olimpiki inafunguliwa katika muda wa chini ya wiki tatu.

Kamari ya Macron yashindwa kumlipa

Macron aliishangaza Ufaransa, na wengi katika serikali yake, kwa kulivunja bunge baada ya chama cha National Rally kuibuka kidedea katika uchaguzi wa bunge la Ulaya nchini humo. Macron alihojo kuwa kuwarudisha wapiga kura vituoni kungeipa Ufaransa "mwelekeo."

Soma pia: Ufaransa: Chama cha National Rally mguu sawa kuchukua hatamu

Rais huyo alikuwa akicheza kamari kwamba kwa kuiweka hatima ya Ufaransa mikononi mwao, wapiga kura wangeviacha vyama vya mirengo mikali ya kulia na kushoto na kuvichagua vyama vya jadi vya mrengo wa kati - ambako Macron alipata uungwaji mkono mkubwa uliompa ushindi wa urais mwaka 2017 na tena mwaka 2022. Hilo, alitumaini, lingeimarisha urais wake kwa miaka mitatu iliyobaki madarakani.

Lakini badala ya kumuunga mkono, mamilioni ya wapiga kura kote kwenye upande wa kushoto na kulia wa mazingira ya kisiasa ya Ufaransa yanayozidi kuwa na mgawanyiko walitumia uamuzi wake wa mshangao kama fursa ya kuonyesha hasira zao kwake.

Chanzo: Mashirika