1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi DRC kufanyika Desemba 20

28 Novemba 2022

Uchaguzi wa rais, wabunge wa kitaifa na kimkoa pamoja na washauri wa wilaya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, utafanyika tarehe 20 Desemba 2023 pamoja na changamoto za kiusalama.

https://p.dw.com/p/4KAVx
Kongo | Demokratische Republik Kongo DRC Soldaten
Picha: Guerchom Ndeb/AFP/Getty Images

Ndivyo ilivyotangazwa na Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (CENI), ikitoa Jumamosi tarehe mbalimbali za mchakato wa uchaguzi, huku ikisisitiza bado kuna vikwazo. Lakini  muungano wa upinzani wa Lamuka unapiga tarehe hizo ukidai kuandaliwe mpango utakaotokana na makubaliano ili kuepuka machafuko.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (CENI), Denis Kadima, ambaye alitangaza tarehe za uchaguzi alisisitiza kuwa zote zitaheshimiwa. Usajili wa wapiga kura utaanza mwezi ujao na utachukua siku 30 katika kila eneo la uchaguzi. Uchaguzi kamili utafanyika tarehe 20 Desemba 2023, kama alivyoainisha Denis Kadima, mwenyekiti wa CENI.

Zaidi alisema "CENI inazialika kwa dhati taasisi na wadau nchini kuhusika kwa uwajibikaji katika uendeshaji wa mchakato wa uchaguzi ili ufanikiwe. Nasisitiza kuwa uchaguzi hautachelewa. Baada ya mwezi mmoja tutaanza kuorodhesha wapiga kura."

Hali tete ya usalama ni miongoni mwa vikwazo vya uchaguzi DRC

DRC Goma Grenzzwischenfall
Wafanyabiashara mpakani mwa DRC na RwandaPicha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Licha ya azma ya CENI kuweza kuandaa uchaguzi katika muda unaoruhusiwa kikatiba, vikwazo vilivyobainishwa mwezi Februari bado viko, ila CENI inategemea  wadau ili kuvishinda. Miongoni mwa vikwazo hivyo ni ukosefu wa usalama unaoendelea katika baadhi ya maeneo ya nchi hii.

Serikali ya Kongo inaendelea na kazi ili kurejesha usalama, kama alivyoeleza Patrick Muyaya, waziri wa mawasiliano na msemaji wa serikali. "Tunaendelea kufanya kazi ya kurejesha usalama tukitumika kijeshi na kidiplomasia. Jumuiya ya kimataifa inalo jukumu la kuturuhusu kurejesha amani mashariki mwa nchi na tunatumai kuwa itafanyika haraka ili wakazi wa upande huo wa nchi waweze kuorodheshwa na kupiga kura."

Upinzani unapinga tarehe za uchaguzi na kushinikiza mabadiliko

Muungano wa upinzani wa Lamuka hauungi mkono hata kidogo tarehe hizo za uchaguzi. Badala yake, unahitaji washikadau mchakato wa uchaguzi kukaa pamoja ili  kurekebisha na hivyo kufikia makubaliano kuhusu tarehe za uchaguzi, na hivyo kuepuka ulaghai, mkanganyiko na haswa  machafuko. Ndivyo alivyoeleza Prince Epenge, mmoja wa wasemaji wa Lamuka. "Kadima anapanga kufanya chaguzi nne kwa siku moja katika nchi kubwa kama Kongo. Anaamua peke yake kuwapangia Wakongo wa ugenini wapige kura akichagua tena peke yake nchi husika, bila kushirikisha vyama vya siasa. Yaani kuna mengi ya kurekebisha kupitia maridhiano baina ya wadau."

Soma zaidi:Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufanya uchaguzi mkuu Desemba 2023.

Kwa mara ya kwanza kabisa, Wakongo wanaoishi ugenini  watapiga kura katika uchaguzi wa urais tarehe 20 Desemba 2023, wakiwemo wale wanaoishi nchini Afrika Kusini, Ubelgiji, Kanada, Marekani na Ufaransa.

DW, Kinshasa.