1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UhamiajiUbelgiji

Ubelgiji yakabiliwa na mzozo wa wakimbizi wasio na makazi

6 Septemba 2023

Ubelgiji ilitangaza wiki iliyopita kuwa haitatoa tena makazi kwa wanaume wanaotafuta hifadhi nchini humo wakiwa pekee yao kutokana na nafasi chache, na sasa wanapaswa kuweka kipaumbele kwa familia, wanawake na watoto.

https://p.dw.com/p/4VzmE
Belgien | Asyl | IND-Antragszentrum in Ter Apel
Picha: Eva Plevier/ANP/IMAGO

Shirika kuu la haki za binadamu barani Ulaya pamoja na vikundi kadhaa vya misaada vimelaani hatua hiyo vikisema inakiuka mikataba ya kimataifa. Kwa muda mrefu sasa Ubelgiji imekuwa ikikosolewa kwa kushindwa kuwapatishia makazi maelfu ya watu ambao wanatafuta hifadhi baada ya kukimbia madhila katika nchi zao.

Hatua ya Ubelgiji ilikabiliwa na ukosoaji kutoka kwa mashirika ya haki za binadamu pamoja na Baraza la mataifa 46 la Ulaya. Akiwasiliana na shirika la habari la AP, Kamishna wa Haki za Binadamu wa Tume ya Umoja wa Ulaya Dunja Mijatovic amesema kukosekana kwa makazi ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kwa wale  wanaoomba hifadhi nchini Ubelgiji, hasa kuhusu haki yao ya kiafya.

Belgien Migranten Hungerstreik
Baadhi ya waomba hifadhi wakiwa wamelala mjini Brussels, UbelgijiPicha: Yves Herman/REUTERS

Milolongo ya watu wanaolala barabani katika mahema nje ya Ofisi kuu ya kuombea hifadhi huko mjini Brussels imeitia doa haiba ya Ubelgiji ambako ndiko kunakopatikana pia makao makuu ya Umoja wa Ulaya.

Disemba mwaka jana, Mijatovic alizihimiza mamlaka za Ubelgiji kutoa huduma bora zaidi kwa wanaotafuta hifadhi baada ya mamia ya watu kulala nje katika mitaa ya Brussels, matukio ambayo yalishuhudiwa kwa muda mrefu hasa katika majira ya baridi kali.

Jumatano ya Agosti 30, 2023, Waziri anayehusika na waomba hifadhi Nicole de Moor alisema kulikuwa na hatari ya ongezeko la shinikizo kwa makazi ya waomba hifadhi katika miezi ijayo na alilenga kuepuka watoto kujikuta mitaani wakati wa majira ya baridi kali na ndio maana alichukua uamuzi wa kwamba wanaume walio pekee yao wajaribu kutafuta makazi yao wenyewe.

Bi Moor alisema Ubelgiji inajitahidi kadri ya uwezo wake na tayari imetoa msaada mkubwa huku akitoa wito kwa mataifa mengine ya Ulaya kuongeza juhudi katika kuwapokea watu wanaoomba hifadhi.

Kulingana na Shirika la Umoja wa Ulaya la Ukimbizi, waomba hifadhi wanaume walifikia kiwango cha asilimia 70 mnamo mwaka wa 2021. Shirika la kuwahudumia wakimbizi nchini Ubelgiji -Fedasil, limesema mwaka jana, nchi hiyo ilipokea maombi yapatayo karibu 37,000.

Wakimbizi kutoka Ukraine wapewa pia hifadhi Ubelgiji

Mbali ya hao, Ubelgiji inawapa pia hifadhi  wakimbizi wapatao 62,000 kutoka Ukraine kufuatia uvamizi wa Urusi. Mwaka jana pekee, Mahakama nchini Ubelgiji ziliihukumu Fedasil kwa zaidi ya mara 5,000 kwa kushindwa kutoa makazi sahihi kwa waomba hifadhi.

Brüssel Räumung eines von Migranten bewohnten Gebäudes
Polisi wakiwafurusha waomba hifadhi katika jumba walikojiegesha mjini Brussels na lililopewa jina "Le Palais"-15.02.2023Picha: Réseau ADES

Watu takriban 100 ambao ni waomba hifadhi wamejiegesha katika jengo kubwa lililotelekezwa na linalozidi kuchakaa linalopatikana katika mtaa maarufu na wenye ofisi za wizara mbalimbali wa "Rue de la Loi". Hata hivyo Polisi imeamuru watu hao kuondoka eneo hilo.

Amil ambaye ni mkimbizi kutoka Afghanistan mwenye umri wa miaka 30 amesema hawana la kufanya na wala hawajui watakapokwenda ikiwa watafurushwa katika jumba hilo. Mawakili na watetezi wa wakimbizi hao wanasema hatua hii ya kutowapa makazi wanamume walio pekee yao, itazidisha tatizo hilo.

Soma pia: UN: Mapigano ya Sahel yataongeza wakimbizi zaidi Ulaya

Philippe Hensmans, mkurugenzi wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International nchini Ubelgiji amesema hatua hii ya serikali ya Brussels ya kusitisha kutoa makazi kwa wanaume inakiuka kwa kiwango kikubwa haki za binadamu.

Kulingana na takwimu rasmi, idadi ya wakimbizi waliowasili nchini Ubelgiji iliongezeka kwa 8% mwezi Julai 2023 na serikali inasema wengi wao ni kutoka Ukraine, Afrika na Asia na hivyo kutatiza uwezo wa makazi kwa waomba hifadhi katika nchi hiyo ndogo ya Ulaya yenye wakazi milioni 11.6.

(RTRE-APE)