1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano makubwa yafanyika Tunisia kupinga hali ngumu

Zainab Aziz Mhariri: Gakuba, Daniel
18 Januari 2021

Zaidi ya watu 1000 wamekamatwa nchini Tunisia wakati ambapo nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika imekumbwa na ghasia kwa siku kadhaa sasa. Waandamanaji wasema wamechoshwa na hali ngumu ya maisha.

https://p.dw.com/p/3o5RO
Tunesien Protest Zusammenstöße
Picha: Fauque Nicolas/Images de Tunisie/ABACA/picture alliance

Maandamano hayo, yaliyosababisha mapambano kati ya raia na na polisi, yanaendelea wakati Tunisia inaadhimisha miaka 10 ya tangu kufanyika harakati zilizoleta mapinduzi katika demokrasia na ikiwa ni miaka 10 tangu muuzaji wa matunda na mboga wa eneo la Manzel Bouzaine alipokufa kwa kujiwasha moto mbele ya jengo la serikali kupinga kudhalilishwa na polisi ambao walikamata shehena kubwa ya bidhaa zake. Mpaka sasa kwa Watunisia wengi hali ya maisha yao haijabadilika. Hasira ya umma inapanda kutokana na kukithiri ukosefu wa ajira huku huduma za serikali zikiendelea kuwa duni.

Soma zaidi:Tunisia yakabiliwa na mgogoro mwingine wa kisiasa

Wizara ya Mambo ya Ndani imesema waandamanaji walikusanyika kwenye barabara za mji mkuu wa nchi hiyo,Tunis na pia kwenye miji mingine ambapo maandamano hayo baadae yalibadilika na kuwa ghasia pale waandamanaji walipopambana na vikosi vya polisi.

Msemaji wa wizara ya mambo ya Ndani Khaled Hayouni amesema, walinda usalama walikabiliwa na makundi ya vijana yaliyojumuisha watu 20 hadi 30. Hayouni amesema kuwa kiwango cha vurugu kilikuwa cha juu.

Msemaji huyo hakuafiki kuyaita hayo kuwa ni maandamano, bali alisema kitendo cha uhalifu na uporaji ambapo baadhi ya walinda usalama walijeruhiwa vibaya.

Waamdamanaji kwenye eneo la Sidi Bouzid mojawapo ya maeno yanayokabiliwa na hali ngumu mno ya kiuchumi
Waamdamanaji kwenye eneo la Sidi Bouzid moja wapo ya maeno yanayokabiliwa na hali ngumu mno ya kiuchumi Picha: Riadh Dridi/AP Photo/picture alliance

Waandamanaji waliingia mabarabarani huku wakiwa wamekaidi amri ya kuwataka wabakie majumbani na kutotoka nje kwa muda wa siku nne, iliyowekwa tangu siku ya Alhamisi iliyopita kwa ajili kupunguza kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona. Waandamanaji wamesema wameamua kufanya hivyo tangu siku ya Ijumaa wiki iliyopita kupinga hali ngumu ya kiuchumi.

Maandamano hayo yalisambaa baada ya video kuwekwa mtandaoni wiki iliyopita iliyomwonesha afisa wa polisi akimshambulia mchungaji wa mifugo. Vurugu hizo ziliisababisha Wizara ya Ulinzi kupeleka vikosi vya jeshi katika miji ya Sousse, Bizert, Kasserine na Siliana kuwasaidia polisi na pia kulinda mali za raia na za serikali.

Soma zaidi:Tunisia yatangaza kuunda baraza jipya la mawaziri

Taarifa zinafahamisha kwamba katika mji mkuu wa Tunis, polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kutawanya waandamanaji. Video zimesambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinazowaonesha waandamanaji wakiwa wamefunga barabara na kuchoma matairi wakati polisi walipokuwa wakijaribu kuwatawanya waandamanaji hao.

Maandamano hayo yanafanyika wakati ambapo Tunisia inatimiza miaka 10 baada ya maandamano ya wanaharakati wa kutetea demokrasia ambapo liliibuka vuguvugu kubwa lililomwangusha rais wa muda mrefu wa nchi hiyo Zine El Abidine Ben Ali.

Tangu wakati huo, Tunisia imetumbukia kwenye hali mbaya ya kiuchumi inayochangiwa na vurugu na pia mashambulio yanayoendeshwa na makundi ya wapiganaji. Janga la corona nalo limezidi kuudhoofisha uchumi wa Tunisia.

Vyanzo:/DPA/RTRE