1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya IEBC Kenya yafanyia majaribio mfumo wake wa matokeo

Thelma Mwadzaya, Nairobi9 Juni 2022

Tume ya uchaguzi nchini Kenya imeanza kufanya majaribio ya mfumo wa teknolojia ya kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu.

https://p.dw.com/p/4CUTA
Kenia Wahlwiederholung | Chef der Unabhängigen Wahlkommission (IEBC) Wafula Chebukati
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Abdul Azim

Shughuli hii inapaswa kuanza zikiwa zimesalia siku 60 kabla ya uchaguzi mkuu.Wakati huohuo, wabunge wamekamilisha vikao vya muhula huu na watarejea kwenye mijadala iwapo litatokea la dharura.Kwa upande mwengine, matokeo ya uhakiki wa daftari la wapiga kura yatakuwa bayana tarehe 16 mwezi huu.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya zoezi hilo kuanza, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya , IEBC, Wafula Chebukati alisisitiza kuwa azma ni kuwa na uchaguzi huru na haki.

Uidhinishwaji wagombea wa uchaguzi Kenya wakamilika

Alhamisi ndiyo siku ya mwisho ya tume ya IEBC kufanya majaribio, kuhakiki na kuitumia teknolojia itakayotumiwa kutangazia matokeo ya uchaguzi mkuu wa Agosti.

Azma ni kuzipekua changamoto na mapungufu ya mfumo ya elektroniki wa kutangaza matokeo ya uchaguzi yatakayotumika kukusanya yale ya mwanzo katika kituo kikuu cha kuhesabu kura cha Bomas of Kenya. 

Tume ya IEBC inajiandaa kuanza shughuli ya kuratibu vituo vya kupigia na kuhesabia kura mintarafu huduma za mtandao wa 3G.
Tume ya IEBC inajiandaa kuanza shughuli ya kuratibu vituo vya kupigia na kuhesabia kura mintarafu huduma za mtandao wa 3G.Picha: Reuters/T. Mukoya

Kisheria, tume ya uchaguzi inalazimika kuthibitisha matokeo hayo kupitia fomu maalum kabla ya kutangaza washindi.Itakumbukwa kuwa mfumo wa teknolojia wa kutangaza matokeo ya uchaguzi ulianza kutumiwa rasmi mwaka 2013 baada ya vurugu za baada ya uchaguzi wa 2007.

Ruto aitaka tume ya IEBC kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru

Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, matokeo ya uchaguzi wa rais yanayonakiliwa kwenye fimu ya 34A yanalazimika kutangazwa kielektroniki kwa kituo kikuu na vile vya maeneo bunge vya kuhesabia kura. Tume ya IEBC inajiandaa kuanza shughuli ya kuratibu vituo vya kupigia na kuhesabia kura mintarafu huduma za mtandao wa 3G.

Kwa upande wake, kampuni ya uhakiki ya KPMG, inayolitathmini daftari la wapiga kura itaweka matokeo yake bayana ifikapo tarehe 16 mwezi huu.Kulingana na IEBC wapiga kura wamefikia milioni 22.5 idadi iliyoongezeka kutokea milioni 19.7 mwaka 2017.

Baadhi ya waliokuwa waangalizi katika uchaguzi wa mwaka 2017 nchini Kenya akiwemo Thabo Mbeki, rais wa zamani wa Afrika Kusini (katikati).
Baadhi ya waliokuwa waangalizi katika uchaguzi wa mwaka 2017 nchini Kenya akiwemo Thabo Mbeki, rais wa zamani wa Afrika Kusini (katikati).Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Yote hayo yakiendelea, bunge la taifa limekamilisha vikao vyake kwa muhula huu japo linaweza kukutana itokeapo dharura. Baadhi walitumia fursa hiyo kuagana na kuwashukuru wapiga kura.

Baraza la Senate linatazamiwa kuhitimisha vikao vyake wiki inayofuatia.Kwavile huu ni mwaka wa uchaguzi, vikao vya bunge vilivurugwa na shughuli za maandalizi kwani kampeni zilianza rasmi mwishoni mwa Mei na wabunge ndio wadau wakuu.

Kadhalika mageuzi ya sheria za uchaguzi hayatafanyika kwani yalitupwa nje kwasababu ya kuwasilishwa kuchelewa. Kwa mantiki hii sheria zilizotumika katika uchaguzi ulipota ndio zitakazotumika.

Thelma Mwadzaya,DW Nairobi.