1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uidhinishwaji wagombea wa uchaguzi Kenya wakamilika

Admin.WagnerD8 Juni 2022

Tume ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya IEBC inajiandaa kusikiliza malalamishi ya wagombea walioshindwa kupata ridhaa ya kuwania nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao. Makaratasi ya kura yataapishwa mwezi ujao

https://p.dw.com/p/4CQd2
Kalonzo Musyoka Kenia Vize Präsident
Picha: AP Photo

Tume ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya, IEBC inaanza rasmi mchakato wa kusikiliza malalamishi ya wagombea wa nyadhifa mbali mbali walioshindwa kupata ridhaa kushiriki. Kulingana na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati,kamati yake ya kusuluhisha mizozo ya uchaguzi itasikiliza malalamishi hayo kuanzia Alhamisi kwa siku kumi zijazo.

"Uhakiki wa hati za wagombea unakamilika tarehe 8 na kuanzia tarehe 9 muda wa kusikiliza malalamishi utaanza rasmi kwa siku 10 zijazo.Watakaotaka kwenda mahakamani wako huru ila ifikapo mwisho wa mwezi tutaanza kuandaa karatasi za kupigia kura.”

Baadhi ya walalamishi watakaolazimika kwenda mahakamani wamepewa muda wa kiasi ya wiki mbili kabla ya masuala yao kusikilizwa tena na kamati ya usuluhishi ya IEBC. Shughuli hii inafanyika baada ya mchakato wa kuhakiki hati za wagombea wa nafasi zote kukamilika.

Kenia Nairobi Wahlvorbereitungen
Makaratasi ya kupigia kura kuanza kuchapishwa JulaiPicha: Reuters/T. Mukoya

Ifikapo tarehe 20 mwezi huu wa Juni, tume ya uchaguzi itajiandaa kuandaa orodha rasmi ya vituo vya kupigia na kuhesabu kura. Karatasi za kupigia kura yamepangwa kuanza kuchapishwa mwezi ujao baada ya daftari la wapiga kura kusafishwa.

Yote hayo yakiendelea,kura mpya ya maoni inaashiria kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga na mgombea wake mwenza Martha Karua wanaongoza kwa 42%. Wapinzani wao wakuu wa muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na naibu wa rais William Ruto na mgombea wake mwenza Rigathi Gachagua wako katika 38% ya uwezo wa kushinda uchaguzi.

Ifahamike kuwa Kenya itakuwa na idadi ndogo zaidi ya wagombea wa urais tangu mfumo wa vyama vingi vya kisiasa kuzinduliwa mwaka 1992. Kufikia sasa ni wagombea 4 tu waliopata ridhaa ya kuwania urais kutoka kwa tume ya uchaguzi na mipaka ya Kenya IEBC. Orodha hiyo ilianza na wagombea 54 waliochujwa hadi 18 na hatimaye wamesalia 4. Raila Odinga wa azimio la umoja One Kenya,William Ruto wa Muungano wa Kenya Kwanza,George Wajackoyah wa chama cha Roots na David Mwaure wa Agano ndio watakaomenyana kwenye kinyanganyiro cha urais. Mwaka 2017 , 8 walijitosa kwenye uchaguzi wa urais sawia na uchaguzi uliotangulia wa 2013. Wakati mfumo wa vyama vingi vya kisiasa ulipoanzishwa,1992, 8 walitaka kushiriki uchaguzi wa rais.

Thelma Mwadzaya, DW Nairobi.