1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya Haki za Binadamu yenye makao yake makuu mjini Geva yashutumiwa kukumbatia serikali dhalimu duniani.

Charles Hilary28 Aprili 2005

Wanachama 53 wa Tume ya Haki za Binadamu yenye makao yake makuu mjini Geneva,wameshutumiwa vikali kutokana na kuzikumbatia serikali dhalimu wakati wa kuchagua wanachama wake.Lakini hata hivyo pendekezo la kuichukulia hatua Tume hiyo bado limezingirwa na mizengwe.

https://p.dw.com/p/CEFx

Hoja hiyo ya shutuma imetoka zaidi katika mataifa ya Magharibi na vikundi vingine vya kutetea haki za binadamu,ambavyo vilirusha tuhuma kwa nchi wanachama wa tume ya haki za binadamu,kama Sudan,Cuba,Jamhuri ya Kidemeokrasi ya Kongo na Zimbabwe na zaidi kwa kuchaguliwa kwa Libya kama mwenyekiti wa Tume hiyo kwa kipindi cha mwaka jana.

Nae Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Kofi Annan,alitoa shutuma zake hadharani kwa wanachama wa Shirika la Umoja wa Mataifa la haki za binadamu ambao wanataka kuchukua nafasi ya Tume hiyo ya Haki za Binadamu ya Geneva.Shirika hilo linachotaka ni kwa Tume ya Haki za Binadamu ibadilishwe na kazi zake kufanywa na kikundi kidogo cha baraza la haki za binadamu.

Iwapo Bwana Annan anayo njia yake,uanachama wa shirika jipya la haki za binadamu litakuwa ni kwa ajili ya serikali tu, na labda wengi wakitoka mataifa ya Magharibi,ambao wanafuata kwa makini kile kinachoitwa kiwango cha juu cha haki za binadamu.

Lakini mawazo yake hayo,ikiwa ni sehemu ya mapendekezo ya kuufanyia mageuzi Umoja wa Mataifa,kuna swali litajitokeza juu ya uwanachama wa bara jipya na mamlaka yake.

Nae Norman Solomon,mkurugenzi mtendaji wa Taasisi inayojishughulisha na utoaji habari za uhakika,yenye makao yake mjini Washington,amependekeza kuwa Marekani ambayo inaonekana kuwa mstari wa mbele kutoa maamuzi yanayoihusu dunia,kwa niaba ya mataifa mengine,isiruhusiwe kutoa mapendekezo yake juu ya uundwaji wa Baraza jipya,kutokana na yenyewe kuwa mstari wa mbele katika uvunjaji wa haki za binadamu chini ya kisingizio cha kupambana na ugaidi.

Akihutubia mkutano wa mwaka wa Tume ya Haki za Binadamu mjini Geneva mapema mwezi huu,Bwana Annan alipendekeza kuwa wanachama wa Baraza jipya ni lazima wachaguliwe na wingi wa robo tatu ya kura miongoni mwa wanachama 191 wa Baraza la Kuu la Umoja wa Mataifa.

Ameongeza kueleza kuwa wale wote watakaochaguliwa ni lazima wawe wenye rekodi nzuri ya kujitolea kwa kiwango cha juu cha haki za binadamu.

Bwana Annan amesema kuwa Tume ya Haki za Binadamu ya Geneva sio tu imepoteza heshima yake,lakini pia imeyumbisha heshima ya Umoja wa Mataifa kwa ujumla.

Mapendekezo hayo ya Bwana Annan pia yameungwa mkono na wanachama 25 wa Umoja wa Ulaya.Lakini mataifa kadhaa yaliyoendelea yameonesha kuwa na mashaka.

Mathalan Jim Paul Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Ulimwengu linalosimamia sera,lenye makao yake makuu New York,amehoji nafasi ya Uingereza katika Baraza hilo jipya,kutokana na yale inayoyafanya Ireland ya Kaskazini.Pia Russia imeshutumiwa kwa kuvunja haki za binadamu katika jimbo lenye mzozo la Chechnya,ambapo waasi huko wanapigania kujitenga.

Amegusia halikadhalika hoja ya Marekani ya kupambana na ugaidi.Anasema sheria ya ugaidi iliyopitishwa mwaka 2001 ikiwa na lengo la kupambana na vitendo vya kigaidi ambayo inatoa ruhusa ya kwa vyombo vya dola kupekua na kukamata mali,kwa ujumla imekuwa ikikiuka katiba na faragha ya mtu pia haki ya mtu kulindwa.

Kwa vyovyote kutokana na hoja zote hizo,Baraza jipya la kusimamia Haki za Binadamu,uundwaji wake na mamlaka yake utabakia kuonekana namna litakavyo kuwa na maingiliano na vikundi visivyo vya kiserikali katika kutekeleza kazi zake.