1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi: Hatuwezi kufanya mazungumzo na Rwanda

Jean Noël Ba-Mweze
31 Januari 2024

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo amerejelea msimamo wake kwamba hakuna mazungumzo yanayowezekana na nchi jirani Rwanda anayoituhumu kufadhili uasi mashariki mwa Kongo.

https://p.dw.com/p/4bsBs
Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: Isa Terli /AA/picture alliance

Rais Tshisekedi ameyasema hayo jioni ya jana wakati akikutana na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao mjini Kinshasa, ambapo alisisitiza kwamba hakuwezi kuwepo na majadiliano yoyote kuhusu uhuru na mamlaka ya Kongo. 

Akitoa matamshi hayo mjini Kinshasa jana Jumanne, Rais Tshisekedi alisema kuwa jeshi la Kongo litawasaka maadui mahali popote walipo na bila kujali gharama.

"Serikali inakumbusha haki na wajibu wake wa kuchukua hatua zote muhimu ili kulinda mamlaka na uhuru wa nchi yetu na pia kulinda wananchi pamoja na mali zao. Hakuna mwenye haki ya kuizuia. Kwa hiyo, mimi kama kamanda mkuu wa jeshi letu, nahakikisha tena kwamba tutatumia nguvu zote ili kuondoa vikosi vya Rwanda kwenye eneo letu," ameeleza Tshisekedi.

Soma pia: Tshisekedi apendekeza nafasi rasmi ya msemaji wa upinzani 

Rais Tshisekedi pia aliishukuru Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, SADC, kwa kutuma vikosi vyake mkoani Kivu Kaskazini ili kuliunga mkono jeshi la Kongo.

Wanadiplomasia waiunga mkono Kongo

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo na mwanadiplomasia mkuu wa Marekani Antony Blinken
Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo na mwanadiplomasia mkuu wa Marekani Antony BlinkenPicha: Evelyn Hockstein/Pool via AP/picture alliance

Kwa upande wao, wanadiplomasia walionesha nia yao kuona Kongo ikiinuka na kwa hiyo wanatamani kuiunga mkono, kama alivyoeleza Martin Chungong Ayafor, Balozi wa Cameroon akiwa pia mkuu wa mabalozi waliopo hapa Kongo, ambaye alimsifia Rais Tshisekedi kwa dhamira yake.

"Ulibaini haja ya kulinda mshikamano wa kitaifa ukijipa jukumu la kupiga vita chuki, ukabila na mambo mengine yanayopinga maadili. Pia ulitoa wito kwa upinzani ukieleza kuwa upinzani unayo nafasi yake katika kipindi hiki cha miaka mitano."

Soma pia:  Umoja wa Mataifa waonya kukithiri kwa matamshi ya chuki DRC

Mkutano huu wa jana na wanadiplomasia umefanyika ikiwa ni siku chache baada ya Félix Tshisekedi kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili wa miaka mitano.

Wakati huo huo, baadhi ya maeneo ya mkoa wa Kivu Kaskazini bado yapo chini ya udhibiti wa waasi wa M23 wanaodhaniwa kuungwa mkono na Rwanda, ilhali huko Kivu Kaskazini, watu 12 waliuawa jana Jumanne katika eneo la Beni ambapo baadhi ya vijiji vilishambuliwa na wanamgambo wa ADF.