1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi asema waasi wa M23 hawajaondoka Rutshuru

Saleh Mwanamilongo
18 Januari 2023

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo Felix Tshisekedi amesema waasi wa M23 bado hawajaondoka katika maeneo ambayo waliyateka jimboni Kivu ya Kaskazini.

https://p.dw.com/p/4MM24
Rais wa Kongo Felix Tshisekedi ameishutumu tena Rwanda kuwaunga mkono waasi wa M23
Rais wa Kongo Felix Tshisekedi ameishutumu tena Rwanda kuwaunga mkono waasi wa M23Picha: Giscard Kusema

Rais Felix Tshisekedi amewashutumu waasi wa M23 kukaidi zoezi la kuwaondoa wapiganaji wake katika maeneo walioyakamata mtaani Rutshuru, jimboni Kivu ya Kaskazini.

''Waasi wa M23, kundi la kigaidi linaloungwa mkono na Rwanda, wanaendelea kuyadhibiti maeneo walioyakamata kwa Kongo. Licha ya shinikizo kutoka jumuiya ya kimataifa, kundi hilo linaonyesha kama linaondoka katika maeneo liliyoyateka, huku lakini likizungukazunguka na kuwaweka wapiganaji wake katika maeneo mengine ya miji linayoishikilia.'', alisema Tshisekedi.

Viongozi wa nchi za kanda la Maziwa Makuu walipitisha makukubaliano mnamo Novemba ambayo kundi la waasi wa M23 lilikusudiwa kujiondoa katika miji liliyonyakua kufikia Januari 15. Hatua hiyo ilikuwa sehemu ya juhudi za kumaliza mzozo ambayo umewahamisha watu wasiopungua 450,000 na kuzua mgogoro wa kidiplomasia kati ya Kongo na nchi jirani ya Rwanda.

Mapema mwezi Januari, ripoti ya ujasusi wa ndani wa Umoja wa Mataifa ilisema haikuwezekana kuthibitisha madai ya M23 kujiondoa katika baadhi ya maeneo kutokana na kuendelea kwa harakati za mapigano,na uchanganuzi wa ripoti hiyo ulionyesha kuwa waasi wa M23 walimekamata maeneo mapya mahali pengine.

Makubaliano ya Luanda

 Waasi wa M23 walitangaza kujiondoa kwenye mjiji ya Kibumba,Rumangabo na Kishishe
Waasi wa M23 walitangaza kujiondoa kwenye mjiji ya Kibumba,Rumangabo na KishishePicha: picture-alliance/ dpa

Tshisekedi aliishutumu tena Rwanda kwa kuchochea mzozo huo na kuunga mkono waasi hao wa M23 tuhuma iliyotolewa pia na baadhi ya nchi za Magharibi na wataalam wa Umoja wa Mataifa, lakini Rwanda inakanusha vikali tuhuma hizo.

Hatua ya hivi karibuni ya kuondoka kwa M23 kutoka miji ya Kibumba,Rumangabo na Kishishe ilitangazwa na jeshi la kanda ya Afrika Mashariki tangu Desemba na mwanzoni mwa mwezi Januari.

Msemaji wa M23 Lawrence Kanyuka amekanusha madai hayo ya Rais Tshisekedi, akisema serikali ya Kinshasa ndio inayokiuka usitishaji wa mapigano. Kanyuka pia aliituhumu serikali kwa kuendelea kuvipa silaha vikundi vya wapiganaji huko mashariki mwa Kongo.

Mashirika kadhaa ya kiraia yameandamana leo mjini Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu ya Kaskazini kupinga ucheleweshaji wa hatua ya kuondoka kwa wapiganaji wa M23. Hata hivyo mamlaka za mji zilipiga marufuku maandamano hayo.