1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi amtaja Kagame "adui" wa Kongo

Jean Noël Ba-Mweze
5 Desemba 2022

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Félix Tshisekedi amewataka Wakongo kutowachukia Wanyarwanda ambao amewataja kama ndugu zao na kusisitiza kuwa adui wa Kongo ni Rais Paul Kagame wa Rwanda na utawala wake.

https://p.dw.com/p/4KTlq
DR Kongo Empfang des Präsidenten Tshisekedi für die Fußball Nationalmannschaft
Picha: Giscard Kusema, Presse- und Kommunikationsdienst des Präsidenten

Huku mvutano huo ukiendelea kati ya marais Paul Kagame wa Rwanda na Felix Tshisekedi wa Kongo, waumini wa Kikatoliki waliandamana jana Jumapili (04.12.2022) kote nchini humo kupinga uchochezi wa Rwanda na unafiki wa jumuiya ya kimataifa. 

Soma Zaidi:DRC na Rwanda zapata mwafaka kuhusu vita mashariki mwa DRC

Rais Félix Tshisekedi alitoa wito huo jana wakati akiwahutubia vijana wa Kongo kupitia ujumbe ulioundwa na mamia ya vijana kutoka mikoa 26 ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo akiwaomba kutofautisha kati ya raia wa Rwanda na utawala wa Rais Paul Kagame.

Tshisekedi alisisitiza kwamba Wanyarwanda  wanahitaji msaada wa Wakongo ili kujikomboa kutoka utawala huo kandamizi.

Alisema "Ni utawala wa Rwanda unaoongozwa na Paul Kagame ndio adui wa Kongo. Wanyarwanda ni ndugu zetu na wanahitaji msaada wetu kwani wamezibwa midomo. Wanahitaji msaada wetu ili kujikomboa, kutukomboa na kuiondoa Afrika mikononi mwa viongozi wa aina hii walio bado nyuma."

Kombibild Felix Tshisekedi und Paul Kagame
Mivutano inazidi kuongezeka baina ya marais wa Kongo, Felx Tshisekedi na Paul Kagame wa Rwanda licha ya hatua za kutafuta amani.

Kauli hizo kali za Rais Tshisekedi zimefuatia shutuma zilizotolewa na Rais Kagame wiki iliyopita ambapo alimshtumu Tshisekedi kwa kutaka kujinufaisha kisiasa kutokana na mzozo unaoendelea mashariki mwa Kongo kwa kuahirisha uchaguzi huku nchi yake ikilaumiwa kwa matatizo hayo.

Wakati huo huo, Wakristo wa Kikatoliki waliandamana mitaani jana Jumapili nchini kote, ili kulaani uvamizi dhidi ya nchi hii unaodaiwa kufanywa na Rwanda kupitia uasi wa M23. Kwa zaidi ya miezi mitano sasa, waasi hao ambao Kinshasa inawataja kama magaidi wanadhibiti mji wa Bunagana na maeneo mengine. Waandamanaji pia walishutumu unafiki wa jumuiya ya kimataifa kama alivyoeleza Padri Bruno Kabambu wa parokia ya Mtakatifu Gabriel.

"Pia tunakemea tabia za baadhi ya mashirika ya kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Jumuiya ya Afrika Mashariki na mengineo ambayo hayana haki. Maumivu ya vita dhidi ya ndugu zetu wa Mashariki yanatulazimu kuwatumia ujumbe wa huruma na mshikamano." Alisema Padri Kabambu.

Soma Zaidi: Waasi wa M23 wajitenga na mapatano ya kusitisha mapigano

Mvutano baina ya Kinshasa na Kigali bado ni wa hali ya juu licha ya juhudi za upatanishi kuongezeka ili kujaribu kuleta amani katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo Umoja wa Mataifa umeinyooshea kidole Rwanda kuwaunga mkono waasi wa M23.

Sikiliza Zaidi: 

Kagame amtuhumu Tshisekedi kutumia mzozo wa M23 kujinufaisha