1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu Truss: Samahamani kwa mokosa lakini siondoki

18 Oktoba 2022

Waziri Mkuu wa Uingereza Liz Truss ameomba radhi kwa "makosa" katika mpango wake uliozusha vurugu kwenye masoko ya kifedha na kuporomosha umaarufu wake, lakini amesema hatoachia ngazi.

https://p.dw.com/p/4IK9u
Britische Premierministerin Liz Truss
Picha: Sean Smith/Getty Images

Truss alitazama kimya bungeni jana Jumatatu wakati waziri wake mpya wa fedha Jeremy Hunt akiuchana chana mpango wa kiuchumi ambao waziri mkuu huyo alikuwa ameupendekeza chini ya mwezi mmoja uliopita, na ambao ulisababisha sokomoko kubwa katika masoko ya kifedha kiasi cha kuilazimu Benki Kuu ya England kuingilia kati kuzuwia mifuko ya pensheni kuporomoka.

Uamuzi wa Truss kuondoa mpango wake umetuliza kiasi shinikizo juu ya gharama za ukopaji za Uingereza, lakini kiwango cha kujirudi kinamaanisha hivi sasa anapigania kusalia katika nafasi hiyo, wiki sita tu baada ya kuchaguliwa kuwa waziri mkuu. Wabunge wachache tayari wameanza kupaza sauti kumtaka ajiuzulu.

UK Schatzkanzler Jeremy Hunt
Waziri wa fedha wa Uingereza Jeremy Hunt akitangaza mpango mpya wa bajeti wa muda mfupi bunge, mjini London, Oktoba 17, 2022.Picha: PRU/AFP

"Sasa natambua kwamba tumefanya makosa, naomba radhi kwa makosa hayo, lakini nimerekebisha makosa, nimemteua waziri mpya wa fedha, tumerejesha utulivu wa kiuchumi na nidhamu ya fedha na ninachotaka kufanya hivi sasa ni kwenda kuwatumikia wananchi. Tulichaguliwa kwenye ilani ya mwaka 2019 na nimejifunga kutekeleza ilani hiyo," alisema Truss katika mahojiano.

Soma pia: Truss aahidi kuiongoza Uingereza kutoka katika kipindi kigumu cha kiuchumi

Madarakani lakini hana mamlaka

Gazeti la Daily Mail ambalo lilisifu mpango wa Truss, lilichapisha kwenye ukurasa wake wa mbele, picha ya waziri mkuu huyo akiondoka bungeni jana chini ya kichwa cha habari kisemacho, "madarakani, lakini siyo mamlakini", huku gazeti jingine linalomuunga mkono la Sun likimuita "Waziri Mkuu Hewa." 

James Heappey, waziri wa ulinzi, amesema leo kuwa mkuu wake Truss, hawezi kumudu kufanya makosa zaidi, lakini akamsifu katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Sky News, kwamba amekiri makosa na kuomba radhi.

Waziri wa fedha Jeremy Hunt, alieteuliwa Ijumaa iliyopita baada ya Truss kumfuta kazi mshirika wake wa karibu Kwasi Kwarteng, akiondoa vipengele vikuu vilivyosalia kwenye mpango wa Truss wa kupunguza kodi jana, ikiwemo kupunguza mpango wake mkubwa wa msaada kwa sekta ya nishati.

England | Parteitag der Konservativen in Birmingham | Kwasi Kwarteng
Waziri wa fedha wa Uingereza aliefutwa kazi Kwasi Kwarteng.Picha: Kirsty Wigglesworth/AP Photo/picture alliance

Truss na Kwarteng walijaribu kurekebisha sera ya fedha ya Uingereza kwa kutangaza punguzo la pauni bilioni 45 katika makato ya kodi ambalo hata hivyo hawakuainisha lingefadhiliwaje, ili kuuondoa uchumi katika mdororo. Lakini mpango huo ulisababisha mtikisiko mkubwa katika masoko ya fedha na kupelekea sarafu ya pauni kushuka kwa kiwango cha chini kabisa dhidi ya dola ya Marekani.

Soma pia: Sarafu ya Uingereza yaanguka dhidi ya dola

Truss alichaguliwa na wanachana wa chama cha Conservative na siyo wapiga kura wote, kwa ahadi ya kupunguza kodi na udhibiti ili kuchochea ukuaji wa uchumi, katika sera ambayo wakosoaji waliitaja kama kurejea kwa mfumo wa miaka ya 1980 uliotumiwa na waziri mkuu wa wakati huo Margaret Thatcher.

Chanzo: Mashirika