1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeremy hunt afuta mipango ya kupunguzwa kodi

17 Oktoba 2022

Je mamlaka ya waziri mkuu Truss yanaelekea wapi wakati miito ikizidi ya kumtaka aondoke madarakani kabla ya kulazimishwa na chama chake kukaa pembeni?

https://p.dw.com/p/4IIMt
England London | Pressekonferenz: Jeremy Hunt
Picha: Tayfun Salci/AP/picture alliance

Waziri mpya wa fedha nchini Uingereza Jeremy Hunt ametangaza mabadiliko makubwa ya kiuchumi katika kile kilichojulikana kama bajeti ndogo ya serikali iliyotangazwa chini ya mwezi mmoja uliopita na mtangulizi wake aliyetimuliwa Kwasi Kwarteng. Hivi sasa waziri huyo mpya ameiondowa mipango mingi ya kupunguza kodi pamoja na matumizi ya serikali.

Jeremy Hunt ametangaza mipango yake hiyo ya kujaribu kuuleta utulivu wa kiuchumi nchini Uingereza baada ya kushuhudiwa kile kilichoitwa bajeti ndogo ya serikali kuvuruga mambo na kusababisha ukosefu wa utulivu katika masoko ya fedha mnamo mwezi Septemba.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari waziri huyo mpya wa fedha Jeremy Hunt amesema anafutilia mbali takriban mipango yote ya kupunguza kodi iliyotangazwa na waziri mkuu Liz Truss pamoja na sera yake ya nishati akibaini kwamba mpango uliopo sasa wa kusaidia katika suala la bei za nishati utaundwa upya katika kutafuta mwelekeo mpya wa kuwasaidia wale hasa wenye uhitaji zaidi kuanzia mwezi Aprili mwakani.

''Ni utaratibu tulioundeleza kwa dhati wahafidhina,utaratibu ambao nauunga mkono kwamba watu wanapaswa kuwa na pesa zaidi wanazopokea katika mshahara.Lakini katika wakati ambapo masoko yanahitaji uhakika  wa kuwa na uwezo wa kuendelea kusimamia fedha za umma,sio sawa kukopa kwa ajili ya kufadhili mipango ya  kupunguza kodi.Kwahivyo nimeamua kwamba kiwango cha msingi cha kodi ya mapato kitabakia kwenye asilimia 20 na kitabakia hivyo kwa muda usiojulikana mpaka hali ya uchumi itakapoturuhusu kuiondowa.''

Tschechien Prag | Britische Premierministerin Liz Truss
Picha: Alastair Grant/Getty Images

Waziri huyo wa fedha wa Uingereza pia ametahadharisha kwamba matumizi ya serikali yatalazimika kupunguzwa katika maeneo kadhaa ili kuleta uthabiti wa kiuchumi nchini. Lakini  wakati mabadiliko hayo ya kisera yakionesha kutuliza masoko ya fedha kwa upande mwingine yanahujumu zaidi mamlaka ya waziri mkuu Liz Truss ambayo toka hapo yanatetereka na kushuhudiwa miito ikiongezeka ya  kumtaka ajiuzulu kabla ya chama chake cha Conservative kilichogawika kuchukua hatua ya kumlazimisha kuondoka.

Kimsingi tangazo la mabadiliko makubwa ya kisera hutolewa kwanza bungeni na waziri mkuu  lakini mara hii ni tafauti waziri wa fedha  Hunt ametangaza mabadiliko hayo baada ya kufikiwa makubaliano na spika wa bunge na tangazo hilo pia limetolewa wiki kadhaa mapema kabla ya muda aliokuwa amepanga. Jeremy Hunt aliteuliwa ijumaa iliyopita baada ya waziri mkuu Truss kumtimua mtangulizi wake Kwasi Kwarteng aliyekalia nafasi hiyo kwa muda wa chini ya wiki sita.

England | Parteitag der Konservativen in Birmingham | Kwasi Kwarteng
Picha: Kirsty Wigglesworth/AP Photo/picture alliance

Ingawa kilichosababisha mtikisiko katika masoko ya fedha na kuporomoka vibaya pauni ya Uingereza ni hatua ya pamoja ya waziri mkuu Truss na Kwasi Kwateng ya kutangaza bajeti ndogo ya serikali ya pauni bilioni 45 ya kusimamia mpango wa kupunguza kodi. Sakata hili limemvunja nguvu waziri mkuu Truss na wabunge wa chama chake wanatafakari juu ya kumuondowa.

Mwakilishi wa serikali bungeni Penny Mordaunt leo hii atajibu swali la dharura bungeni kuhusu kufutwa kwa waziri wa fedha Kwarteng baada ya chama cha upinzani Labour kutoa ombi hilo na spika kuridhia. Chama hicho kilishamtaka waziri mkuu Liz Truss kutoa tamko juu ya kuondolewa huko kwa waziri wa fedha lakini ofisi yake ikasema  Mordaunt ambaye anasimamia shughuli za serikali bungeni ndiye atakayetowa jibu.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW