1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump: Marekani "itaimiliki" Gaza

5 Februari 2025

Rais wa Marekani Donald Trump amesema Marekani "itachukua udhibiti" na kuumiliki Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4q2VB
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu (kushoto) akizungumza na Rais Donald Trump (kulia)
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu (kushoto) akizungumza na Rais Donald Trump (kulia)Picha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Trump aliyasema haya wakati alipokuwa mwenyeji wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Jumanne kwa ajili ya mazungumzo muhimu ya usitishaji mapigano na wanamgambo wa Hamas.

Endapo hilo la Marekani kuimiliki Gaza litafanyika,basi hatua hiyo itakuwa imeivunja sera ya miongo kadhaa ya Marekani kwa mzozo wa Israel na Palestina.

Jeshi la Marekani kusaidia katika ujenzi

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano huo na Netanyahu, Trump vile vile alirudia kauli yake kwamba Wapalestina wanastahili kuondoka Gaza iliyoharibiwa vibaya kwa vita na wakaanze maisha mapya ya kudumu katika mataifa mengine ya Mashariki ya Kati kama Misri na Jordan, licha ya Wapalestina na mataifa hayo mawili yote kulikataa pendekezo hilo.

Ukanda wa Gaza ulioharibiwa vibaya kutokana na vita vya Israel dhidi ya Hamas
Ukanda wa Gaza ulioharibiwa vibaya kutokana na vita vya Israel dhidi ya HamasPicha: OMAR AL-QATTAA/AFP

Rais huyo wa Marekani alisema Marekani itaisafisha Gaza kwa kuyaondoa mabomu ambayo hayajalipuka na kuleta ustawi wa kiuchumi ambao utabuni ajira na makao chungunzima kwa watu watakaoishi katika eneo hilo.

Trump vile vile aliongeza kwamba haondoi uwezekano wa kupeleka jeshi la Marekani kusaidia katika ujenzi mpya wa Gaza.

Ila wakati mmoja Trump alionekana kuashiria kuwa si Wapalestina watakaorudi kuishi Gaza akidai, "eneo hilo halistahili kujengwa upya na kukaliwa na watu wale waliolipigania na kuishi maisha mabaya katika ardhi hiyo," alisema Trump.

Rais huyo wa Marekani lakini hakujibu swali la vipi na kwa mamlaka gani Marekani itaichukua Gaza na kuikalia kwa muda mrefu.

Alisema atafanya ziara Gaza, Saudi Arabia na Israel inagwa hakuweka wazi ni lini atakapofanya ziara hiyo.

Hatua ya kuwaondoa kwa nguvu Wapalestina kutoka Gaza huenda ikawa ukiukwaji wa sheria ya kimataifa na itapingwa vikali sio tu Mashariki ya Kati bali na marafiki wa Marekani walioko Magharibi.

Mara tu baada ya kikao hicho cha Trump na Netanyahu na waandishi wa habari, Saudi Arabia katika taarifa ilisisitiza kukataa hatua ya kuondolewa kwa Wapalestina kutoka kwenye ardhi yao.

Mpango utakaoibadili historia

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alimsifu Trump kama "rafiki mkubwa zaidi" ambaye Israel imewahi kuwa naye.

Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Jim Watson/AFP/Getty Images

Netanyahu alisema mpango wa Trump kwa Gaza unaweza kuibadili historia na ni mpango muhimu wa kutazamwa kwa karibu.

Mbali na hayo Trump alisema kwamba angependa kuingia kwenye makubaliano na Iran ili kuimarisha mahusiano ya nchi hizo mbili ila akaongeza kwamba kwa hilo kufanyika basi Tehran isiunde silaha za nyuklia.

Ama kuhusiana na vita vinavyoendelea Ukraine, Trump alisema kwa sasa utawala wake unafanya mazungumzo na Urusi pamoja na Ukraine na kwamba mazungumzo hayo yanaendelea vyema.

Netanyahu ndiye kiongozi wa kwanza wa kigeni kufanya ziara White House tangu Trump achukue uongozi yapata wiki mbili zilizopita.

Vyanzo: DPAE/AFP/AP/Reuters