Benjamin Netanyahu anaelekea Marekani kukutana na Trump
2 Februari 2025Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameelekea leo nchini Marekani ambapo atakuwa kiongozi wa kwanza wa kigeni kukutana na Rais Donald Trump tangu kuapishwa kwake mwezi uliopita.
Kwa mujibu wa ofisi ya Netanyahu baada ya kukamilika kwa duru ya nne ya kubadilishana wafungwa ni kwamba mazungumzo kati yake na Trump yatajikita katika kuanza mazungumzo ya awamu ya pili ya kusitisha mapigano huko Gaza. Hata hivyo tarehe rasmi ya mazungumzo yanayohusisha wapatanishi na wajumbe kutoka Hamas na Israel bado haijawekwa wazi huku awamu ya kwanza siku 42 ikitarajiwa kukamilika mwezi ujao.
Soma zaidi.Israel yasema imewaua magaidi huko Ukingo wa Magharibi
Baada ya usitishaji vita kuanza kutekelezwa Gaza mwezi uliopita baada ya miezi 15 ya vita, Trump alipigia debe mpango wa "kusafisha" eneo la Gaza na kutoa wito kwa Wapalestina kuhamia nchi jiranikama vile Misri na Jordan.
Msimamo ambao wachambuzi wa siasa wanasema umeimarisha hitaji la Netanyahu la kuwa na uhusiano thabiti wa Marekani wakati ambapo anakabiliwa na shinikizo la ndani ya Israel na la kikanda.