Trump azidi kuandamwa
1 Oktoba 2019Wakati Trump akimshambulia vikali mbunge wa chama cha Democratic Adam Schiff na kusema anatakiwa kukamatwa kwa kile alichokitaja "uhaini", Australlia nayo imethibitisha kwamba rais huyo hivi karibuni alimuomba waziri mkuu wa nchi hiyo na viongozi wa mataifa mengine kumsaidia mwanasheria mkuu wa Marekani William Barr kupata taarifa zitakazomsaidia kuufanya uchunguzi wa mshauri maalumu Robert Muller kutiliwa shaka.
Robert Muller aliongoza uchunguzi wa uingiliaji wa Urusi kwenye uchaguzi mkuu wa Marekani wa mwaka 2016.
Trump pia hakuacha kuwashambulia watoboa siri ambao madai yao yalihusu mawasiliano yake ya simu na rais wa Ukraine Volodymir Zelensky mwezi Julai, yamesababisha kuanzishwa kwa uchunguzi wa bunge linalodhibitiwa na chama cha Democratic wa kumshitaki.
Mwanasheria wake binafsi, Rudy Giuliani, anatajwa kuwa sehemu muhimu ya juhudi za kuiomba Ukraine kufanya uchunguzi dhidi ya familia ya mpinzani mkuu wa Trump kwenye uchaguzi ujao Joe Biden, ambayo haijatuhumiwa kwa kufanya kosa lolote lile.
Hapo jana alipofanyiwa mahojiano na kituo cha utangazaji cha Fox, kuhusiana na hati hiyo ya bungem Giuliani alisema anatafakari hatua atakazozichukua:"Ninapima njia mbadala. Nitakusanya ushahidi wangu wote pamoja na mawasiliano ya ujumbe. Sijui, ikiwa wataniruhusu nitumie kanda za video na mawasiliano niliyorekodi. Nilikusanya ushahidi huu wote kabla ya uchunguzi wa Mueller kumalizika, kwa hivyo ilikuwa wazi kuwa jukumu langu kama wakili wa Rais, mkutano wa mwisho ambao Waukraine waliuitisha, nililifanya wakati uchunguzi ulipomalizika.''
Mwenyekiti wa kamati ya bunge ya masuala ya kijasusi, Adam Schiff pamoja na wenyeviti wa kamati nyingine mbili zinazoongozwa na wademocratic zimetoa hati hiyo kwa Giuliani na kumpa hadi Oktoba 15 kuwa amewasilisha nyaraka hizo.
Huko Australia, msemaji wa serikali amethibitisha alipozungumza na kituo cha utangazaji cha ABC kwamba Trump aliwasiliana na waziri mkuu Scott Marrison kuomba kumsaidia mwanasheria mkuu Bill Barr kupata taarifa zinazohusiana na uchunguzi wa Muller.
Kulingana na gazeti la New York Times, lililowanukuu maafisa wawili wa Marekani ambao hawakutambulishwa, nakala ya maandishi ya mawasiliano hayo ilitolewa tu kwa kundi dogo la wasaidizi wa Trump ambao wanataka udhibiti mkali wa mawasiliano hayo.
Australia imesema iko tayari wakati wote kusaidia juhudi za kufungua njia kwenye uchunguzi wa masuala kadhaa na waziri mkuu huyo pia alikubali kufanya hivyo.
Uchunguzi mpya wa maoni uliochapishwa jana umeonyesha kwamba Wamarekani wamegawika juu ya ama kuunga mkono mashitaka dhidi ya Trump ama kujiweka pembeni.