1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sakata dhidi ya Trump na tuhuma za ngono laibuka tena

Isaac Gamba
3 Mei 2018

Meya wa zamani wa New York,  Rudy Giuliani amesema Rais Donald Trump alimlipa muigizaji wa filamu za ngono Stormy Daniels kiasi cha dola 130,000 kupitia kwa aliyekuwa mshauri wake binafsi wa masuala ya kisheria.

https://p.dw.com/p/2x5iz
US-Präsident Donald Trump
Picha: picture-alliance/RS/MPI/Capital Pictures/M. Theiler

Akizungumza jana na kituo cha matangazo ya televisheni cha Fox , Rudy Giuliani amesisitiza kuwa malipo hayo yanaelekea kutaka kuhalalishwa kisheria. 

" Fedha hizo hazikuwa kwa ajili ya kampeni na niwaeleza ukweli ambao hamuufahamu, kwani hakuna kampeni inayogharamia mambo yanayokiuka kanuni za uchaguzi" amesema Giuliani.

Kauli ya Giuliani kuwa malipo  hayo hayahusiani na kampeni inaibua utata kutokana na ukweli kwamba ukimya wa nyota huyo wa filamu za ngono ulipatikana siku chache kabla kampeni za mwaka 2016 na katika kipindi ambacho Trump alikuwa akishughuka zaidi na kutoa ufafanuzi baada ya kuvuja kwa mikanda ya vidio ikimuonesha Trump akijisifu kwa kitendo chake cha kuwadhalilisha wanawake kingono.

Hata hivyo, Richard L. Hassen mhadhiri wa masuala ya sheria za uchaguzi kutoka Chuo Kikuuu cha Irvine cha California  anasema iwapo malipo hayo yalikuwa ni ya binafsi basi hakutakuwa na ukiukaji wa taratibu za kampeni kiuchaguzi.

Ama kwa upande mwingine hoja ambayo inaweza kutolewa na serikali ni kuwa malipo hayo kwa muigizaji Daniels ya dola 130,000 yaliyofanywa na Cohen yalikuwa ni mkopo kwa ajili ya timu ya kampeni ya Trump ili kuendelea kufanya tuhuma hizo kuwa siri.

Na iwapo Trump atamlipa tena Cohen fedha hizo basi ijulikane kuwa yalikuwa ni matumizi kwa ajili ya kampeni na ambayo pia hata hivyo yangepaswa kufahamika kwa tume ya uchaguzi.

 

Gharama za kampeni zinapaswa kujulikana kwa tume ya uchaguzi

USA Rudy Giuliani
Rudy Giuliani Meya wazamani wa New YorkPicha: picture-alliance/dpa/Sipa Pool/B. Anthony

Gharama zote za kampeni ikiwa ni pamoja na malipo pamoja na mikopo zinapaswa kujulikana kwa tume ya taifa ya uchaguzi.

Hasen anasema swali ambalo lilikuwepo kabla ya jana Jumatano ni iwapo Cohen alifanya malipo kwa ajii ya timu ya kampeni ya Trump ambayo hayakuripotiwa.

Anasema iwapo hilo ni kweli inaonekana kama mshauri wa masuala ya kisheria wa Trump  Michael Cohen anaweza kuwa ametumia fedha hizo kama mkopo kwa timu ya kampeni ya Trump badala ya kutoa fedha hizo kama mchango.

Iwapo itakuwa ni hivyo basi hizo ni habari nzuri kwa Cohen kwani sasa itakuwa ni jukumu la rais au timu yake ya kampeni kutoa taarifa juu ya mkopo huo na siyo jukumu la  Cohen.

Wachambuzi wanasema kuwa  umuhimu wa suala hili ni kuwa linamuhusisha moja kwa moja rais na iwapo Trump anafahamu juu ya malipo hayo basi  sasa tutakuwa tunazungumzia suala ambalo linahusiana na kampeni za uchaguzi na ambalo ni suala zito".

Naye Norm Eisen aliyekuwa ni mshauri wa masualaya kisheria katika kitengo cha maadili katika ikulu ya White House wakati wa utawala wa Barack Obama na ambaye mara kadhaa amekuwa akimkosoa Trump anasema rais huyo angepaswa kuweka wazi mkopo huo wakati alipoweka wazi taarifa zake kifedha.

Haikufahamika mara moja meya huyo wa zamni wa New York anataka kufaidika na nini kutokana na kuweka wazi taarifa ambazo awali hazikujulikana na pia inaweza kuhusishwa na taarifa kuwa mshauri huyo wa zamani wa masuala ya kisheria wa Trump, Michel Cohen hivi sasa anahojiwa na Shirika la Upelelezi la Marekani, FBI.

Mwandishi: Isaac Gamba/APE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo