1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aonya nchi kutofanya biashara na Iran

7 Agosti 2018

Rais Donald Trump wa Marekani ameyaonya mataifa kutofanya biashara na Iran, huku akisifu vikwazo vipya dhidi ya taifa hilo, alivyovitaja kuwa vikali zaidi kuwahi kuwekwa dhidi ya Iran. 

https://p.dw.com/p/32kkr
USA Donald Trump zum Atomdeal mit Iran
Picha: Reuters/J. Ernst

Rais Donald Trump wa Marekani hii leo ameyaonya mataifa kuacha kufanya biashara na Iran, huku akisifu vikwazo vipya dhidi ya taifa hilo, alivyovitaja kuwa vikali zaidi kuwahi kuwekwa dhidi ya Iran, hatua iliyoibua mchanganyiko wa ghadhabu, hofu na uasi nchini Iran. 

Mapema hii leo rais Trump aliandika kupitia ukurasa wake wa twitter kwamba vikwazo dhidi ya Iran tayari vimekwishawekwa. Hivi ni vikwazo vikali zaidi kuwahi kuwekwa, na mwezi Novemba watatangaza tena vikwazo vingine, aliongeza Trump.

Aliongeza kuwa, yoyote anayefanya biashara na Iran hatafanya biashara na Marekani, na kwamba anachokitafuta ni amani duniani, na si zaidi ya hapo.

Muda mfupi tangu kuanza kutekelezwa kwa vikwazo hivyo, kampuni ya magari ya Ujerumani ya Daimler ikasema itasimamisha biashara zake nchini Iran. Msemaji wa Daimler amesema kwenye taarifa yake kwa shirika la habari la AFP kwamba wamesitisha shughuli zao nchini Iran kutokana na vikwazo hivyo vilivyoanza kutekelezwa, na kuongeza kuwa Daimler itaendelea kufuatilia kwa karibu hatua za kisiasa.

Iran Teheran Bankautomaten
Wairan wengi wanailaumu serikali yao kwa kurejeshwa kwa vikwazo hivyo.Picha: picture-alliance/AA/F. Bahrami

Wairan wengi, ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara wa magari wanailaumu serikali yao kwa kurejeshwa  vikwazo hivyo vya Marekani, lakini pia wanahofia huenda vikawa ni pigo la mwisho kwenye uchumi wa taifa hilo unaoyumba. 

Kujiondoa kwa Trump kwenye mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 hapo mwezi Mei tayari kuliwaogopesha wawekezaji na kuchochea kushuka kwa thamani ya sarafu ya Irani ya rial, kabla hata ya vikwazo hivyo vinavyohusiana na nyuklia kuanza kutekelezwa upya.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif amewaambia waandishi wa habari kwamba namna ambavyo dunia imeijibu hatua hiyo ya Trump, imeonyesha kwamba Marekani imetengwa kidiplomasia.

Iran Dollar- und Rial-Banknoten in einer Wechselstube in Teheran
Masoko ya fedha yamefunguliwa, baada ya kufungwa kwa miezi mitano. Picha: Reuter/R. Homavandi

Mmoja wa wafanyakazi wa sekta ya ujenzi amesema akiwa katika mtaa mmoja mjini Tehran kwamba anajisikia kama maisha yake yamevurugika. Vikwazo hivyo tayari vimekwishaathiri kwa kiasi kikubwa maisha ya watu. Mfanyakazi huyo amesema hawezi hata kununua chakula, wala kulipa kodi ya nyumba.

Serikali za Ulaya zimeeleza kughadhabishwa na mkakati huo wa Trump, unaosababisha biashara zao zilizopo Iran kukabiliwa na kitisho cha kuadhibiwa kisheria na Marekani. Waziri wa masuala ya Mashariki ya Kati kwenye ofisi ya mambo ya nje nchini Uingereza, Alastair Burt ameliambia shirika la utangazaji la Uingereza, BBC kwamba Wamarekani wamekosea.

Maduka ya kubadilisha fedha kote nchini Iran yamefunguliwa hii leo kwa tahadhari, baada ya kufungwa kwa miezi mitano, kufuatia hatua ya Marekani ya kujiondoa kwenye mkataba huo wa nyuklia na kwa kiasi kikubwa kauthiri uchumi wa Iran.

Wafanyabiashara wawili ambao hawakutaka kujitambulisha kwa kuwa hawakuruhusiwa kuzungumza na waandishi wa habari, wameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba viwango vya awali huenda vikawa ni rial 93,000 kwa dola moja, ikiwa ni pungufu kutoka rial 98,000 kwa dola, iliyouzwa kwenye masoko ya kilanguzi usiku wa jana.

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE/APE/AFPE.

Mhariri:Iddi Ssessanga