1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaUturuki

Tetemeko la ardhi: Juhudi za uokoaji zaingia siku ya nne

Sylvia Mwehozi
10 Februari 2023

Waokoaji wanaendelea na juhudi za kufukua vifusi kuwatafuta manusura, siku nne baada ya tetemeko la ardhi ambalo limewaua watu karibu elfu 22,000 nchini Uturuki na Syria huku nchi kadhaa zikiendelea kutoa misaada.

https://p.dw.com/p/4NK7X
Türkei Erdbeben Rettungskräfte in Kahramanmaras
Picha: Mustafa Seven/AA/picture alliance

Msaada wa kwanza wa Umoja wa Mataifa ulifanikiwa kuwasili jana katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi nchini Syria lakini matumaini ya kuwapata manusura zaidi yamefifia tangu zipite siku tatu ambazo wataalamu wanazingatia kama kipindi muhimu cha kuokoa maisha ya binadamu. Msafara wa Umoja wa Mataifa uliobeba misaadaulivuka mpaka wa Uturuki na kuingia eneo la Kaskazini Magharibi mwa Syria linaloshikiliwa na waasi, ikiwa ndio njia pekee ya kuwafikia raia bila ya kupitia maeneo yanayothibitiwa na vikosi vya serikali ya Syria. Soma: Idadi ya vifo Uturuki na Syria yapindukia 20,000

Erdbeben Syrien Aleppo Rettungskräfte aus Armenien
Waokoaji wakiwatafuta manusura katika kifusi cha jengo lililoporomoka kaskazini mwa mji wa Aleppo nchini SyriaPicha: AFP

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha ufunguzi wa njia mpya ya kuvuka mpaka kwa ajili ya misaada ya kiutu baina ya Uturuki na Syria. Hali ya baridi kali katika mji wa Uturuki wa Gaziantep uliopo karibu na kulikotokea tetemeko la ardhi, imeshuka hadi chini ya nyuzi joto tatu mapema leo Ijumaa. Licha ya baridi hilo kali, maelfu ya familia zinalazimika kulala ndani ya magari au mahema ya muda huku wazazi wengine wakionekana kuwabeba watoto wao kwenye mablanketi na kurandaranda mitaani.

Siku nne baada ya mkasa huo mbaya, miujiza bado inaonekana kwa baadhi ya watu kuokolewa wakiwa hai kutoka chini ya vifusi. Katika mji wa Antakya, msichana wa miaka 10 ameokolewa usiku wa leo akiwa hai. Katika jimbo la Hatay nchini Uturuki, watu 9 wamegundulika kuwa hai baada ya kukwama kwenye jengo kwa muda wote.Idadi ya vifo yapindukia 17,000 baada ya tetemeko la ardhi katika mpaka kati ya Uturuki na Syria

Sita kati yao wameokolewa na kazi ya kuwaokoa walionaki inaendelea. Kwingineko katika mji wa Uturuki wa Diyarbakir, mwanamke mmoja ameokolewa ikiwa ni zaidi ya masaa 100 tangu litokee tetemeko la ardhi na waokoaji wanaendelea na juhudi za kumsaka mtoto wake.  Raia mmoja mkaazi wa Syria ambaye amepoteza familia yake yote anasimulia. "Ndugu wa familia yangu wote wamekufa: baba yangu, mama, kaka, dada na mpwa. Siamini hili! siamini kabisa! jana tuliweza kuwavuta mama na kaka yangu wakiwa wamekufa na leo tumeipata miili ya dada, mpwa na baba yangu".

Misaada zaidi yatolewa

Für Artikel: DW Middle East - Assad nutzt Erdbeben politisch aus
Msafara wa Umoja wa Mataifa uliobeba misaada umewasili SyriaPicha: OMAR HAJ KADOUR/AFP/Getty Images

Benki ya dunia imesema kuwa itatoa dola milioni 1.78 kwa ajili ya Uturuki wakati Marekani ikitaja kiasi cha dola milioni 85 kama usaidizi wa dharura wa kiutu kwa ajili ya Uturuki na Syria. Tangazo la Marekani kupitia shirika lake la maendeleo la USAID, limetolewa muda mfupi baada ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken kuzungumza na mwenzake wa Uturuki  Mevlut Cavusoglu.

Serikali ya Syria, ambayo iko chini ya vikwazo vya nchi za Magharibi, imetoa wito wa msaada wa Umoja wa Mataifa huku ikisema misaada yote lazima ifanywe kwa uratibu wa pamoja na Damascus na kupitishiwa ndani ya Syria lakini sio mpaka wa Uturuki.

Siku ya Ijumaa rais wa Syria Bashar al-Assad ametembelea hospitali ya chuo kikuu cha Aleppo ikiwa ndio ziara yake ya kwanza iliyoripotiwa katika eneo lililokumbwa na tetemeko. Taarifa ya ofisi ya rais imeonyesha picha za Assad na mkewe wakiwasalimu majeruhi wa mkasa huo.