1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania, Uganda zakubaliana kuimarisha biashara, uwekezaji

10 Mei 2022

Tanzania na Uganda zimekubaliana kuondoa vizingiti visivyo vya kodi kati yao ili kuinua biashara na uwekezaji. Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa ziara ya siku ya rais Samia Suluhu Hassan nchini Uganda.

https://p.dw.com/p/4B6ZS
Uganda Präsidentin Samia Suluhu Hassan
Picha: Uganda’s ministry of Foreign Affairs

Hatua ya kuondoa vizingiti hivyo maarufu kama NTBs inafuatia majadiliano kati ya maafisa wa ngazi za juu kutoka Tanzania na Uganda waliokutana mwezi Januari mwaka huu.

Marais hao wawili wameagiza kwamba maafisa watendaji wawe wakikutana kila mwezi kuona kwamba vizingiti vyovyote vinavyojitokeza vinashughulikiwa ili kuimarisha biashara kati ya nchi hizo mbili na pia Afrika Mashariki.

Miongoni mwa kero kubwa kwa wafanyabiashara nchini Uganda na katika mataifa ya Afrika Mashariki imekuwa ada inayotozwa magari ya mizigo hii ikiwa dola 520 kwa kila gari ya kigeni inayopitia barabara za Tanzania.

Uganda Präsidentin Samia Suluhu Hassan
Rais Samia Suluhu Hassan akiwaburudishwa baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Entebbe, Mei 10, 2022.Picha: Uganda’s ministry of Foreign Affairs

Lakini sasa magari yatakuwa yakitozwa dola kumi tu kwa kila kilomita mia moja ikimaanisha kuwa kati ya Mutukula na Dar Es Salam umbali wa kilomita 1,500 za barabara yatalipa  dola 150 za Kimarekani.

Pande zote  aidha zimekubaliana kuruhusu  shehena ya sukari ya tani 10,000 kuuzwa Tanzania ili kuziba upungufu wa bidhaa hiyo nchini humo.

Wakati huohuo, Uganda itasambaza nyaya ya umeme kuweza kukidhi mahitaji katika mikoa ya hadi Mwanza. Pia Tanzania itagiza bidhaa za matibabu zinazotengenezwa Uganda.

Taarifa ya mkurugezi wa mawasiliano ya ofisi ya rais wa Tanzania, ilisema madhumuni ya ziara hiyo ni kuimarisha na kudumisha zaidi historia iliyopo na mahusiano ya kidiplomasia pamoja na ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizo mbili.

Taarifa hiyo iliitaja ziara hiyo kuwa ya kwanza ya kiserikali kufanywa na Rais Samia tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani mwezi Machi 2021.