1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Taliban: Haki za wanawake wa Afghanistan ni suala la ndani

29 Juni 2024

Serikali inayoongozwa na kundi la Taliban nchini Afghanistan imesema mahitaji ya haki za wanawake ni masuala nchi hiyo inayopaswa kutatua.

https://p.dw.com/p/4hfPi
Afghanistan | Shambulio kwenye msikiti huko Herat
Askari wa usalama wa Taliban wakiwa wamesimama huku Waafghanistan wakiomboleza katika maziko ya Waislamu wa Kishia waliouawa baada ya watu wenye silaha kushambulia msikiti katika wilaya ya Guzara mkoani Herat Aprili 30, 2024.Picha: Mohsen Karimi/AFP/Getty Images

Tamko hilo limetolewa kuelekea mkutano unaoongozwa na Umoja wa Mataifa kujadili hali ya Afghanistan ambako suala la kutowajumuisha wanawake katika mkutano huo limekosolewa vikali.

Serikali hiyo ya Taliban iliyowawekea vikwazo wanawake tangu ilipochukua madaraka mwaka 2021, itatuma wajumbe wake katika mazungumzo ya duru ya tatu yatakayofanyika Qatar kuanzia kesho Jumapili.

Wawakilishi wa mashirika ya kiraia yakiwemo mashirika ya kutetea haki za wanawake watahudhuria mkutano huo wa kesho. Wawakilishi hao baadaye wanatarajiwa kuwa na mkutano mwengine na wajumbe wa kimataifa wakiwemo maafisa wa Umoja wa Mataifa baada ya kumaliza mkutano wao rasmi.

Makundi hayo yamekosoa hatua ya kutowajumuisha wanawake wa Afghanistankatika mkutano huo na kutokuwepo kwa masuala ya haki za binaadamu katika ajenda.

Hata hivyo msemaji wa serikali ya Taliban Zabihullah Mujahid ameuambia mkutano wa waandishi habari mjini Kabul kwamba serikali inatambua masuala ya wanawake, ambayo ni mamabo yanayopaswa kujadiliwa na waafghanistan wenyewe.