1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Taiwan yapuuza vitisho vya China

Angela Mdungu
4 Aprili 2023

Taiwan imepuuzia mbali vitisho vya China muda mfupi kabla ya mkutano unaotarajiwa kati ya Rais Tsai Ing-wen na spika wa bunge la Marekani Kevin MacCarthy hapo kesho Jumatano

https://p.dw.com/p/4PgvB
Taiwan Taoyuan | Präsidentin Tsai Ing-wen vor der Abreise in die USA
Picha: Sam Yeh/AFP/Getty Images

Taiwan imepuuzia mbali vitisho vya China muda mfupi kabla ya mkutano unaotarajiwa kati ya Rais Tsai Ing-wen na spika wa bunge la Marekani Kevin MacCarthy hapo kesho Jumatano. Ikumbukwe kuwa Wiki iliyopita, China ilitishia kuwa itachukua hatua kama Rais wa Taiwan Tsai Weng atakutana na spika wa bunge la Marekani.

Rais wa Taiwan Tsai Wang amekuwa akitembelea nchi za Belize na Guatemala ambazo ni washirika wake katika bara la Amerika ya kati. Sehemu muhimu ya safari yake itakuwa ni kukutana na spika wa bunge la Marekani Kevin McCarthy mjini Los Angeles, wakati akijiandaa kurejea nyumbani. China inaiona Taiwan kuwa ni sehemu yake na inachukulia mikataba na shughuli zozote kati ya Marekani na maafisa wa Taiwan kama  changamoto kwa serikali yake.

Ziara ya Rais Tsai ina nia ya kuonesha kuwa serikali yake inaungwa mkono kimataifa. Belize na Guatemala ni mataifa mawili pekee kati ya nchi 13 zinazoitambua rasmi Taiwan. Idadi ya nchi hizo imeporomoka kutokana na shinikizo la China na fedha inazozielekeza kwa nia ya kukitenga kisiwa hicho.

China: Tunafuatilia yanayoendelea

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya China katika mkutano na waandishi wa habari mapema leo alisema kuwa, China itafuatilia kwa karibu yanayoendelea nna italinda kwa uthabiti mipaka yake. 

Soma zaidi:Marekani kuidhinisha mpango wa uuzaji wa silaha kwa Taiwan

Nayo wizara ya mambo ya kigeni ya Taiwan imesema kwamba haijawahi kuwa sehemu ya China na kwamba ukosoaji wa hivi karibuni wa China ni upuuzi.

Spika wa bunge la Marekani Kevin McCarthy
Spika wa bunge la Marekani Kevin McCarthyPicha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Hata hivyo China imekuwa ikirudia madai yake kwa Taiwan, licha ya kuwa Taiwan inaendeleza mfumo wake wa serikali ya kidemokrasia tangu pande hizo mbili zilipotengana baada ya vita ya wenyewe kwa wenyewe ya mwaka 1949. Imeendeleza pia shinikizo lakijeshi ambapo, jeshi la ukombozi lilituma ndege 20 za kivita kati ya Jumatatu na Jumanne wiki hii sambamba na meli za kivita zikifanya mazoezi ya kijeshi ambayo yameongezeka kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni.

Ziara ya Tsai nchini Marekani itafanyika ikiwa ni wiki moja baada ya Honduras kutangaza kuwa inavunja mahusiano na Taiwan na kuiunga mkono China. Hatua hiyo huenda imechochewa na mradi wa bwawa la kufua umeme Honduras, lililojengwa na kampuni kutoka China.

Chanzo: APE/AFPE