1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Taiwan yaanza mazoezi ya ufyatuaji mizinga

Sylvia Mwehozi
9 Agosti 2022

Jeshi la Taiwan limeanza mazoezi ya ufyatuaji wa mizinga katika hatua ya kujilinda dhidi ya shambulio lolote wakati China nayo ikiendelea na Luteka zake licha ya tangazo la kukamilisha mazoezi hayo siku ya Jumapili.

https://p.dw.com/p/4FIIA
Taiwan | Militär führt Artillerieübungen durch
Picha: Annabelle Chih/Getty Images

Taiwan imesema kuwa mazoezi hayo ya kijeshi yanafanyika katika eneo la kusini mwa nchi na yalianza usiku wa Jumanne yakihusisha urushaji wa mizinga. Wiki iliyopita, China ilizindua mazoezi makubwa ya kijeshi karibu na Taiwan, katika hatua ya kujibu ziara iliyofanywa na Spika wa bunge la Marekani Nancy Pelosi kisiwani humo. Pelosi amekuwa afisa mwandamizi wa Marekani kuzuru kisiwa hicho kinachojitawala ndani ya miongo kadhaa.

Taiwan inaishi chini ya tishio la mara kwa mara la uvamizi wa China, ambayo inachukulia kisiwa hicho kama sehemu ya himaya yake. Kwenye taarifa yake, jeshi la Taiwan limedai kuwa Luteka hizo zilikuwa tayari zimepangwa na hazijafanywa kama hatua ya kuijibu China.

Awali China, ilikuwa imetangaza kwamba Luteka zake za kijeshi karibu na Taiwan zitamalizika Jumapili, lakini hadi kufikia Jumatatu iliendelea na mazoezi ya kijeshi ya baharini na angani na kuzusha wasiwasi juu ya uwezekano wa kuibuka mgogoro katika eneo muhimu kwa biashara ya kimataifa.

Taiwan | Militär führt Artillerieübungen durch
Mizinga ya Taiwan Picha: Ann Wang/REUTERS

Televisheni ya taifa ya China imeripoti kwamba mazoezi hayo yanalenga "operesheni za kupambana na manowari na uvamizi wa baharini" karibu na kisiwa hicho. Rais Joe Biden alisema kuwa hana wasiwasi na Taiwan lakini akaelezea hofu na hatua za China katika ukanda huo. Biden ameongeza kuwa hatarajii hali hiyo kuwa mbaya zaidi..China yafutilia mbali ushirikiano na Marekani kutokana na mzozo wa Taiwan

Wakati huohuo wizara ya uchukuzi na mawasiliano ya Taiwan ilisema siku ya Jumatatu kwamba shughuli za anga huko Taiwan taratibu zimeanza kurejea kawaida baada ya anga linalozunguka kisiwa hicho kufunguliwa tena.

Hapo awali wizara hiyo ilisema safari nyingi za ndege kwenda na kutoka kisiwani ziliendelea kufanya kazi wakati wa mazoezi ya kijeshi ya China yaliyoanza Agosti 4, ikiwa ni wastani wa karibu ndege 150 kuondoka na kuwasili kwa siku. 

Wiki iliyopita China ilituma ndege nyingi na kurusha moja kwa moja makombora karibu na kisiwa wakati wa mazoezi yake ya kijeshi. Mazoezi hayo yalisababisha baadhi ya mashirika ya ndege kusitisha safari za kueleka mjini Taipei na kubadilisha njia za ndege kati ya Asia ya kusini na Kaskazini mashariki ili kuepuka eneo lililoathiriwa.