1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taiwan: Blinken ailaumu China kwa luteka zake za kijeshi

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssessanga
5 Agosti 2022

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema luteka kubwa za kijeshi zilizofanywa na China kukizunguka kisiwa cha Taiwan lilikuwa zoezi lisilo na msingi.

https://p.dw.com/p/4FBq7
Taiwan China Konflikt Manöver
Picha: Huizhong Wu/AP/dpa/picture alliance

Wizara ya ulinzi ya Taiwan imesema jumla ya ndege 68 za kijeshi za China na meli 13 za jeshi la wanamaji ziliendesha luteka katika mlango wa bahari ya Taiwan na kwamba baadhi ya mazoezi hayo ya kijeshi kwa makusudi yalivuka eneo lisilo rasmi linalotenganisha pande mbili hizo. Wizara hiyo imeilaani China. Katika taarifa yake, imesema hatua ya vikosi vya kijeshi vya China ya kufanya luteka katika eneo hilo nyeti imevuruga hali ya utulivu iliyokuwepo na imekiuka sheria kwa kuingia katika eneo la bahari na anga ya Taiwan.

Aliyesimama: Rais wa Taiwan Tsai Ing-wen
Aliyesimama: Rais wa Taiwan Tsai Ing-wenPicha: TAIWAN PRESIDENTIAL OFFICE/REUTERS

Watu wa kisiwa cha Liuqiu, kilichoko kilomita 13 kusini-magharibi mwa kisiwa kikuu cha Taiwan na mojawapo ya sehemu iliyo karibu zaidi na eneo lilikofanyika luteka za kijeshi China, leo Ijumaa wameonesha hisia tofauti kuhusu mazoezi hayo juu ya usalama wao.

Jeshi la China limesema katika taarifa yake kwamba limefanya mazoezi ya anga na baharini kaskazini, kusini magharibi na mashariki mwa Taiwan na linaendelea na luteka hizo ili kupima uwezo wa pamoja wa wanajeshi wake.China ilizindua mazoezi hayo makubwa zaidi ya kijeshi kuwahi kutokea katika bahari na anga karibu na Taiwan hpo jana Alhamisi siku moja baada ya ziara ya Nancy Pelosi katika kisiwa hicho.

Soma Zaidi:China yamuwekea vikwazo Pelosi

Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesema imemwekea vikwazo Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi na familia yake, hata hivyo vikwazo hivyo havijabainishwa. Wizara hiyo imesema ziara ya Pelosi ni uingiliaji mkubwa wa mambo ya ndani ya China. Wizara ya mambo ya nje ya China imesema Beijing pia inasitisha mazungumzo na Washington katika masuala kadhaa muhimu ikiwa ni pamoja na sera ya ulinzi, uratibu, ushirikiano wa kuwarejesha nyumbani wahamiaji haramu na usaidizi wa kisheria katika masuala ya jinai.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony BlinkenPicha: OLIVIER DOULIERY/AFP

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema China inajaribu kubadili utaratibu uliopo katika mlango wa bahari ya Taiwan kwa kufanya majaribio ya makombora na mazoezi ya kijeshi. Amesema ukweli ni kwamba ziara ya Pelosi ilikuwa ya amani na hivyo hakuna uhalali wa hatua hizi zilizopita kiasi. Blinken ameyasema hayo katika mkutano wa baraza la mawaziri wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini-Mashariki ya Asia (ASEAN) katika mji kuu wa Cambodia, Phnom Penh.

Angalia:

Nancy Pelosi awasili Taiwan

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Hua Chunying, amesema China inaitaka Marekani kuacha mara moja kuboresha uhusiano na eneo la Taiwan, na kusimamisha mara moja kuiuzia Taiwan silaha. Amesema ikiwa kweli Marekani inawajibika, ingezuia ziara ya Pelosi ya uchokozi huko Taiwan!. Vilevile Marekani inapaswa kuondoa idadi yake kubwa ya ndege za kijeshi na meli za kivita katika eneo la Asia-Pasifiki.   

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi Picha: Ji Chunpeng/Xinhua/picture alliance

Serikali ya Marekani ilitangaza hapo jana kuwa imeahirisha majaribio yalilyokuwa yamepangwa kwa muda mrefu ya makombora ya masafa marefu ili kuepusha mvutano unaozidi kuongezeka kati yake na China.

Vyanzo:DPA/RTRE