1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan: Waandamanaji watawanywa kwa gesi ya kutoa machozi

Zainab Aziz Mhariri: Tatu Karema
2 Januari 2022

Vikosi vya usalama vimetumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya maalfu ya waandamanaji wanaounga mkono demokrasia nchinin Sudan

https://p.dw.com/p/45433
Sudan Khartum | Demonstration & Protest gegen Militärjunta
Picha: AFP/Getty Images

Watu hao waliandamana Jumapili nje ya ikulu, mjini Khartoum kupinga mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 25 yaliyoongozwa na kiongozi wa kijeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, walipaza sauti wakiimba kuwa wanataka mamlaka yawekwe mikononi mwa raia na waliwataka wanajeshi warudishwe kwenye kambi zao.

Kama ilivyo kila mara yanapofanyika maandamano tangu kufanyika mapinduzi hayo ya kijeshi nchini Sudan, mamlaka imeweka vizuizi barabarani, huku makontena yakitumiwa kuyafunga madaraja yanayouunganisha mji mkuu wa Khartoum na maeneo mengine kupitia kwenye mto Nile.

Waandamanaji katika mji wa al-Daim karibu na mji mkuu wa Khartoum
Waandamanaji katika mji wa al-Daim karibu na mji mkuu wa KhartoumPicha: AFP/Getty Images

Mitandao ya intaneti na simu za rununu hazifanyi kazi tangu asubuhi na vikosi vya usalama vimekuwa vikifanya doria kwenye mji huo mkuu.

Kundi la NetBlocks linalofuatilia mwenendo wa wavuti limesema huduma za mitandao ya simu zilikatwa tangu mapema asubuhi kabla ya muda uliopangwa wa kuanza maandamano hayo ambayo ni ya kwanza katika mwaka huu wa 2022. Wanaharakati hutumia mitandao kwa ajili ya kuandaa maandamano na kusambaza moja kwa moja picha za mikusanyiko hiyo.

Televisheni ya Al Hadath imemnukuu mshauri wa kiongozi wa kijeshi Abdel Fattah Al-Burhan akisema jeshi halitamruhusu mtu yeyote kuiingiza nchi katika machafuko na kwamba maandamano yanayoendelea yanawaathiri watu kimwili, kisaikolojia na kuzidi kuwavuruga kiakili na mwishowe hayataleta suluhuhisho la kisiasa.

Kiongozi wa kijeshi wa Sudan jenerali Abdel Fattah Al-Burhan
Kiongozi wa kijeshi wa Sudan jenerali Abdel Fattah Al-BurhanPicha: Marwan Ali/AP/dpa/picture alliance

Hata hivyo maalfu ya raia wa Sudan walijitokeza kuandamana kuwakumbuka waandamanaji wasiopungua 54 waliouawa katika ghasia tangu mapinduzi.

Wanaharakati wanasema mwaka huu wa 2022 utakuwa mwaka wa kuendeleza upinzani, wameeleza hayo katika machapisho kwenye mitandao ya kijamii.

Wanadai haki kwa watu waliouawa tangu mapinduzi na haki ya zaidi ya watu 250 waliokufa katika maandamano makubwa yaliyoanza mwaka 2019 ambayo yalisababisha kuondolewa madarakani aliyekuwa rais wa Sudan Omar al-Bashir.

Wanaharakati nchini Sudan wamelaani dhulma za kingono wakati wa maandamano ya Desemba 19, ambapo Umoja wa Mataifa umesema wanawake na wasichana wapatao 13 walikabiliwa na ukatili huo.

Wanawake waunga mkono maandamano ya kusaka demokrasia nchini Sudan
Wanawake waunga mkono maandamano ya kusaka demokrasia nchini SudanPicha: Ashraf Idris/AP Photo/picture alliance

Umoja wa Ulaya na Marekani zilitoa taarifa ya pamoja kulaani unyanyasaji huo wa kingono uliotumiwa kama silaha ya kuwazuia wanawake kushiriki kwenye maandamano na pia kuzinyamazisha sauti zao.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, imesema zaidi ya watu milioni 14 wanahitaji msaada wa kibinadamu sawa na raia mmoja kati ya Wasudan watatu anahitaji msaada. Umoja wa Mataifa umesema idadi hiyo ni ya kiwango cha juu zaidi katika muda wa mwongo mmoja.

Vyanzo:AFP/RTRE