1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usitishwaji mapigano Sudan waanza kutekelezwa

23 Mei 2023

Mpango wa kusitisha mapigano kwa wiki moja Sudan umeanza jana usiku wakati mashuhuda katika mji mkuu Khartoum wakiripoti kuziona ndege za kivita zikiruka katika anga za mji huo na kuwepo mapigano katika baadhi ya maeneo

https://p.dw.com/p/4Rgr7
Sudan Khartum | Gepanzertes Fahrzeug der Sudanesischen Armee
Picha: AFP/Getty Images

Mashuhuda waliripoti mapigano kaskazini mwa Khartoum, na mashambulizi ya kutokea angani mashariki mwa mji mkuu huo baada ya saa tatu na dakika 45 usiku wakati mpango huo wa kuwekwa chini silaha ulipoanza kutekelezwa.

Soma pia: Miripuko na majibizano ya risasi yasikika tena Khatoum kabla ya kuanza usitishaji mapigano

Sudan Konflikte Kämpfe
Moshi wafunika anga za Khartoum kutokana na milipukoPicha: AFP

Msururu wa mipango ya awali ya kusitisha mapigano yote ilikiukwa na majenerali wawili wanaozozana, lakini Marekani na Saudi Arabia – ambao walisimamia mpango wa karibuni – walisema huu ni tofauti kwa sababu ulitiwa saini na pande zote na utaungwa mkono na mfumo wa kufuatilia utekelezwaji wake.

Baada ya wiki tano za mapigano makali kati ya jeshi linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan na vikosi vya wanamgambo wa RSF vya Mohamed Hamdan Dagalo, wawakilishi walisaini mjini Jeddah Saudia makubaliano ya kusitisha vita kwa siku saba ili kuruhusu upelekaji wa msaada wa kiutu.

Soma pia: Papa Francis ahimiza amani Sudan

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Sudan Volker Perthes aliliambia jana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa mapigano na shughuli za kijeshi bado vinaendelea, licha ya ahadi kutoka kila upande za kutovuruga utekelezaji wa mpango huo wa kusitisha mapigano "Ni vizuri kwamba mfumo wa ufuatiliaji wa makubaliano hayo umewekwa ambapo itawezekana kusema, kama ikihitajika pia kusema hadharani, ni wapi na lini na nani aliyeukiuka mpango huo. Kama utakiukwa."

Naye mwakilishi wa Sudan AL-HARITH IDRISS AL-HARITH MOHAMED, ambaye ni mtiifu kwa Burhan, aliilaumu RSF kwa ukiukaji unaofanywa nchini humo. "Upeo wa makubaliano hayo unajumuisha Sudan yote, kukomeshwa uhasama, kukoma kuzilenga ndege za kiraia na ndege za msaada wa kiutu, na kukomesha ukusanyaji wa silaha kutoka vyanzo vya kigeni na kukomesha ubomoaji na uharibifu wa miundombinu ya kiraia na vitendo vyote vya uporaji na uharibifu."

Wakati vikosi vya serikali vinadhibiti anga vina askari wachache ardhini katikati ya mji mkuu Khartoum, ambako vikosi vya RSF viko mitaani.

Saa chache kabla ya kuanza kutekelezwa kwa mpango wa kusitisha mapigano, kamanda wa RSF Dagalo alitoa ujumbe wa sauti kwenye mitandao ya kijamii, ambapo alizishukuru Saudi ana Marekani lakini akawahimiza wapiganaji wake kutafuta ushindi. Aidha, alizungumzia ripoti za ukiukaji kutoka kwa wanajeshi wake – ikiwemo uporaji uliokithiri, kuwalenga raia na mashambulizi kwenye makanisa – yote hayo akiwalaumu wale aliowaita "waliopanga njama ya mapinduzi” jeshini. Kwa wapiganaji wake, alisema "ama ni ushindi au kifo cha kishahidi, na ushindi utakuwa wao.”

Mpango huo umeongeza matumaini ya kusitishwa vita ambavyo vimesababisha watu karibu milioni 1.1 kukimbia makao, wakiwemo Zaidi ya 250,000 waliokimbilia nchi Jirani, na kutishia kuiyumbisha kanda nzima ambayo tayari ni tete.

Afp, reuters