1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uongozi wa mpito wa miaka 3 waafikiwa Sudan

Daniel Gakuba
15 Mei 2019

Baraza la kijeshi linalotawala Sudan limefikia makubaliano na vuguvugu la waandamanaji juu ya kuundwa kwa utawala wa mpito wa miaka mitatu kabla ya kukabidhi madaraka kamili kwa utawala wa kiraia.

https://p.dw.com/p/3IVqm
Sudan Demonstration in Khartum
Picha: picture-alliance/AA/M. Hjaj

Pande mbili katika majadiliano hayo, baraza la wanajeshi linalotawala Sudan na vuguvugu la waandamanaji lijulikanalo kama ''muungano kwa ajili ya uhuru na mabadiliko'' zimekubaliana juu ya muda wa miaka mitatu ya utawala wa mpito baada ya mazungumzo ya karibu masaa 12. Awali jeshi lilitaka kipindi hicho kiwe miaka miwili, huku waandamanaji wakipendekeza miaka minne. Tangazo la makubaliano hayo limetolewa na mmoja wa wajumbe wa baraza la kijeshi, LutenI Jenerali Yasser al-Atta.

Sudan - Generalleutnant Shamseddine KabbashiSudan - Generalleutnant Shamseddine Kabbashi
Jeshi la Sudan limesema halina mpango wa kung'ang'ania madaraniPicha: Getty Images/M. El-Shahed

''Makubaliano yamefikiwa kwamba uongozi wa mpito utahudumu kwa miaka mitatu. Miezi sita ya kwanza ya kipindi hicho, itajikita katika kusaini makubaliano ya kusitisha mapigano na makundi ya waasi katika nchi hii.'' Amesema Jenerali al-Atta.

Makundi ya waasi aliyoyataja ni yale katika maeneo ya vita, kama Darfur, Blue Nile na Kordofan ya Kusini.

Kinyang'anyiro cha kudhibiti taasisi

Mwanajeshi huyo amesema baada ya kukubaliana juu ya muda huo, hivi sasa mazungumzo yanatuama juu ya kuundwa kwa taasisi zitakazokuwa mihimili ya uongozi wa mpito, ambazo ni baraza tawala, baraza la mawaziri na bunge lenye viti 300, asilimia 67 ya viti hivyo vikikaliwa na wawakilishi wa vuguvugu la waandamanaji lijulikanalo kwa kifupi ka DFCF.

Uwakilishi katika taasisi nyingine, yaani baraza tawala na baraza la mawazirindio unajadiliwa hivi sasa baina ya jeshi na DFCF. Asilimia 33 ya viti vinavyosalia bungeni, itajazwa baada ya mashauriano katika baraza tawala litakaloundwa.

Jenerali al-Atta ameahidi kuwa katika muda usiozidi masaa 24, makubaliano ya kuunda taasisi hizo zote yatakuwa yamefikiwa na kutiwa saini, katika mazingira na vigezo vinavyokidhi mahitaji ya umma wa Sudan.

Matumaini yenye mashaka

Sudans Präsident Omar al-Bashir
Omar al-Bashir alipinduliwa baada ya kuitawala Sudan kwa miaka 30Picha: Getty Images/A. Shazily

Hata hivyo, waandamanaji mitaani pamoja na kutiwa moyo na tangazo hilo, bado wanayo mashaka. Mmoja wao, Mohammed Abdullah, aliyezungumza na shirika la habari la AFP, amesema kitendawili ni kujua mamlaka itakayosimamia utekelezwaji wa makubaliano yaliyofikiwa.

Kikwazo kikubwa katika mazungumzo ya kuunda taasisi ni kukubaliana juu ya upande utakaokuwa na wajumbe wengi katika kila taasisi, kwa sababu kila upande; majenerali wa jeshi na wanaharakati wa kiraia, unataka kuwa na kauli ya mwisho. Bado maelfu ya waandamanaji wanaendelea kukita kambi mbele ya makao ya jeshi, kulitia kishindo likubali kuachia madaraka liliyojikabidhi baada ya kumuangusha rais wa kiimla Omar al-Bashir tarehe 11 Aprili, aliyetawala kwa mkono wa chuma kwa muda wa miaka 30.

afpe,rtre