Mahasimu Sudan Kusini wachelewa kuunda serikali
7 Mei 2019Wawakilishi wa Rais Salva Kiir na mpinzani wake kiongozi wa waasi Riek Machar wamekubaliana kuchelewesha kuunda serikali ya kugawana madaraka baada ya mazungumzo ya amani kutopiga hatua. Pande hizo mbili zilikutana nchini Ethiopia kwa ajili ya kuufufua mpango wa amani wa mwaka 2018 wenye lengo la kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza mwaka 2013, miaka miwili tangu Sudan Kusini ilipojipatia uhuru wake.
Mwezi Septemba, viongozi wote hao wawili walisaini makubaliano ya kugawana madaraka, ambayo siku ya mwisho kuyatekeleza hayo ni Mei 12. Msingi wa makubaliano hayo yanamtaka Machar arejeshwe katika nafasi yake na makamu wa rais. Lakini suala hilo sasa litacheleweshwa kwa miezi sita.
Taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya ushirikiano wa Maendeleo wa nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, IGAD siku ya Ijumaa imeeleza kuwa pande hizo zimefafanua kwamba vikwazo vya kukosekana kwa nia ya kisiasa, fedha pamoja na muda ni changamoto ambayo imechelewesha kutekelezwa kwa majukumu hayo kabla ya kuundwa kwa serikali ya mpito.
Maafisa katika mazungumzo hayo wamesema kuwa majukumu 59 muhimu ambayo yanahitaji kutekelezwa kabla ya Mei 12, ni 27 tu ambayo yameshakamilika. Mengine 17 yanaendelea kufanyiwa kazi, huku vipengele 15 vikiwa bado havijatathminiwa.
Wasiwasi wa kiusalama wamzuwia Machar kurejea
Wawakilishi wa Machar wamesema kulikuwa na haja ya kuchelewesha hilo kwa miezi sita ili kutatua masuala ya kiusalama pamoja na mambo mengine ambayo yanadaiwa kumzuia kiongozi huyo kurejea Juba kutoka uhamishoni, ambako alikimbilia mwaka 2016 wakati makubaliano ya awali ya amani yalivunjika.
Henry Dawar, mwenyekiti msaidizi wa chama cha Machar cha SPLM-IO anasema uamuzi huo wa kuongeza muda, unazuia kuwepo kwa mawazo yoyote yale ya kuirejesha Sudan Kusini katika vita. Dawar amefafanua kuwa hivi sasa mpango wa amani utatekelezwa na nchi hiyo itakuwa na amani ya kudumu.
Wakati huo huo, serikali imekiri kwamba pande hizo mbili zinarudi nyuma katika suala la kusitisha kabisa mapigano na kukosekana kwa mpangilio wa usalama katika kipindi cha mpito.
Mjumbe maalum wa IGAD nchini Sudan Kusini, Ismael Wais amesema ana matumaini kwamba pande zote hizo zimeuepuka mzozo kwa kukubaliana kufanya kazi zaidi ili kuyapatia ufumbuzi masuala kadhaa ya mkataba huo, kuliko kuendelea kushinikiza kutekelezwa mapema makubaliano hayo.
Wais amebainisha kuwa kila mmoja anajiuliza swali, 'nini kinafuata'? Je kutakuwa na tatizo? Utekelezaji wa makubaliano umeshindikana? Tayari tumeshindwa na maswali ya namna hiyo. Mjumbe huyo wa IGAD anasema mkutano wa sasa wa viongozi wa kisiasa wa Jamhuri ya Sudan Kusini umedhihirisha kuwa vyama vyote bado vina nia ya kuyatekeleza makubaliano ya amani.
Ingawa mkataba wa amani ya Sudan Kusini umepunguza mapigano na kwa kiasi kikubwa kuuondoa mzozo wa kibinaadamu nchini humo, jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa limesema katika ripoti yake iliyotolewa siku ya Jumanne kwamba Sudan Kusini bado inakabiliwa na changamoto kubwa.
Maelfu ya watu wameuawa na wengine mamilioni wamelazimika kuyakimbia makaazi yao kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini.
chanzo: dw